Baada ya kuahirishwa mara tatu, hatimaye Mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), leo unaanza kwa kujadili ajenda tano kubwa, ikiwamo inayosababisha nyufa mpya katika ujenzi wa jumuiya hiyo.
Ni mwelekeo gani jumuiya hiyo inapaswa kuchukua, hasa baada ya kushuhudia kusuasua kwa miradi mikubwa katika umoja huo, ni moja ya masuala makubwa yatakayoibua mijadala mizito katika mkutano huo.
Kuna minong’ono kuwa suala la mwelekeo mpya ambao jumuiya inapaswa kuchukua, limesababisha mvutano kiasi cha kutoelewana kwa baadhi ya wakuu wa nchi wanachama wa EAC, ambayo miaka ya hivi karibuni imekuwa ikishindwa kutosheleza bajeti yake.
Mkutano huo unafanyika wakati nchi wanachama zikiwa zimegawanyika kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Umoja wa Nchi za Ulaya (Epa).
Wakati Kenya na Uganda, kwa upande mmoja, zinasukuma kwa nguvu zote jitihada za kuridhiwa kwa mkataba wa Epa, Tanzania inaongoza kundi linalopinga mkataba huo.
Tanzania imeshatamka rasmi kwamba haitasaini mkataba huo ambao unaruhusu, pamoja na mambo mengine, bidhaa kutoka nchi za Afrika Mashariki kuingia Ulaya bila kodi.
Katika utaratibu huo pia, baadhi ya bidhaa kutoka Tanzania zitaweza kuingia katika ukanda huo bila kutozwa kodi huku baadhi ya bidhaa kodi ikiondolewa taratibu kwa muda wa miaka 25.
Tanzania inauona mkataba huo kuwa unaigawa jumuiya kwa ukoloni mamboleo na kwamba utaua kabisa ubunifu, viwanda vya ndani na kugeuza ukanda huu kuwa wa kuzalishaji malighafi. Tanzania inaamini kwa sasa hakuna mwanachama wa EAC aliye tayari kushindana kiuchumi na nchi za Ulaya.
Septemba mwaka jana, wakuu wa EAC walikutana wakati Tanzania ikionyesha upinzani mkali kwa mkataba huo. Ni katika mkutano huo wa 17 ndipo walikubaliana kuwapa wataalamu wa uchumi kutoka serikali za nchi wanachama muda zaidi wa kuwasiliana ili kuangalia upya misimamo yao na kukutana tena Januari.
Hadi sasa hakuna dalili kwamba nchi hizo zitafikia makubaliano ya pamoja, na tayari Bunge la Tanzania, ambalo kiutaratibu ndilo linaloridhia mikataba yote ya kimataifa, limeshapiga kura kuizuia Serikali kusaini mkataba huo.
Habari kutoka ndani ya vikao vya matayarisho ya mkutano huo wa 18, zinadai kuwa suala la Epa halitarajiwi kupewa kipaumbele. Tanzania imeendelea kusisitiza kwamba nchi za EAC zisisaini Epa mpaka faida na hasara zake zitakapowekwa wazi.
Sudan Kusini
Suala jingine linalotarajiwa kuibua mjadala ni taarifa ya maendeleo yaliyofikiwa katika kuiingiza Sudan Kusini katika EAC. Wakuu hao wataamua kama wakati mwafaka umefika wa kuikubali moja kwa moja nchi hiyo ifikapo Julai mwaka huu.
Tayari Sudan Kusini imeteua wanachama wake wa kujiunga na Bunge la Afrika Mashariki (Eala) na Mahakama ya Afrika Mashariki kama inavyoelekezwa katika mchakato wa kuikubali nchi hiyo.
Marais hao wanatakiwa kutoa mwelekeo kama nchi hiyo inaweza ikateua makamishna wa EAC na kutoa majina ya watakaoiwakilisha katika nafasi za kiutendaji ndani ya sekretarieti na jumuiya.
Bajeti ya Jumuiya
Jambo jingine muhimu ni mfumo mahususi wa ugharamiaji bajeti ya Jumuiya. Mawaziri wa jumuiya, isipokuwa Burundi, wamekubaliana kuendelea kwa mfumo wa sasa wa uchangiaji sawa na kuweka vikwazo kwa watakaoshindwa kulipa.
Nguo na viatu vya mitumba
Pia, katika meza ya mkutano wa leo utajadili suala la uzuiaji kwa awamu wa uagizaji wa nguo na viatu vya mitumba, ambao unafanyika kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2016.
Marais pia wanatarajiwa kuipitisha kuwa sheria miswaada mbalimbali iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge la Afrika Mashariki kama wa Mfumo wa Usimamizi wa Forodha, wa Sheria ya Matumizi ya EAC na wa Sheria ya Matumizi ya Ziada ya EAC.
Soko la Pamoja
Wakuu hao wa nchi pia wanatarajiwa kujadili ripoti ya hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Soko la Pamoja, moja kati ya hayo ni kuzitambua kwa pamoja hati za biashara kutoka kila nchi na suala la kuzuia kabisa utozaji kodi mara mbili kwa kampuni zinazofanya biashara kati ya nchi hizo.
Katika mkutano wa hivi karibuni wa Baraza la Mawaziri wa EAC liliiomba Tanzania kuharakisha mchakato wa kupitia upya mfumo wake wa kisheria na kumaliza mawasiliano ya ndani kuhusu ulinganishaji wa ada za vibali vya kazi ifikapo Septemba.
Ombi hilo limekuja kufuatia uamuzi wa hivi karibuni wa Serikali ya Tanzania kupunguza ada ya vibali vya ukaazi hadi dola 500 za Kimarekani kutoka dola 2,000 kwa raia wa Afrika Mashariki wanaotaka kukaa na kufanyakazi nchini.
Kenya, Uganda na Rwanda wamefuta kabisa ada ya vibali vya kazi, lakini Tanzania na Burundi hawajaridhia suala hilo.