Baada ya kamati ya uchunguzi wa makinikia ya madini kutoa ripoti yake juzi, wengi wanaona kuwa Tanzania imekuwa ikiibiwa kiasi kikubwa cha fedha tangu usafirishaji mchanga wa dhahabu ulipoanza takriban miaka 20 iliyopita.
Wako wanaosema kuwa kiwango hicho cha fedha kinachotokana na kati ya tani 7.8 hadi 15 za madini yaliyo katika makinikia hiyo, kingeweza hata kutosheleza mahitaji ya bajeti ya mwaka.
Lakini kwa mujibu wa kanuni za uchimbaji madini, stahiki ya nchi katika madini haiwezi kuzidi asilimia 10 ya mrabaha.
Kamati iliyoundwa na Rais ambayo iliongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma, ilisema imebaini kuwa kampuni ya Acacia, ambayo inaendesha migodi mitatu nchini, haikutangaza madini yote yaliyomo kwenye mchanga huo uliozuiwa bandarini na kwamba kiwango cha dhahabu iliyomo ni kubwa zaidi ya kilichotangazwa.
Wachimbaji wa madini wenye leseni pamoja na kulipa kodi nyingine kwa Serikali kama za mapato na kampuni, hutakiwa na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kulipa mrabaha.
Mrabaha ni malipo yanayofanywa na kampuni inayochimba madini kama fidia ya kiuchumi inayolipwa kwa Serikali kutokana na kuchimba rasilimali zake ambazo hazina mbadala.
Kwa mujibu wa kifungu 87(1) wachimbaji wa urani, almasi ghafi na vito ghafi wanatakiwa kulipa mrabaha wa asilimia tano huku kwa madini kama dhahabu, shaba, fedha na platina wakitoa asilimia nne ya thamani ya madini yote.
Madini mengine ya ujenzi kama mchanga, mawe, chokaa hutakiwa kulipiwa mrabaha wa asilimia tatu wakati vito vilivyokatwa na kuchongwa vikilipiwa asilimia moja.
Matokeo ya kamati yanaonyesha kuwa thamani ya madini yote yaliyopo kwenye makontena 277 ni kati ya Sh829.4 bilioni hadi Sh1.439 trilioni.
Iwapo hesabu ya asilimia nne ya mrabaha itapigwa kwa thamani ya chini iliyoanishwa na kamati ya Sh829.4 bilioni kwa kuzingatia dhahabu, fedha na shaba zina thamani kubwa kuliko madini mengine yaliyoanishwa, basi Serikali ilitakiwa ipate Sh33.17 bilioni.
Ripoti ya kamati ya Profesa Mruma ilijumuisha hesabu za madini yote yenye thamani katika makontena hayo yakiwemo yale ya kimkakati kama lithium inayotumika zaidi duniani kutengeneza betri za vifaa vya kielektroniki kama simu za mkononi.
Na iwapo asilimia hiyo nne itapigwa kwa kiwango cha juu cha thamani ya madini hayo cha Sh1.439 trilioni, Serikali ilitakiwa ipate mrabaha wa Sh57.56 bilioni.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa nyaraka zilizotolewa na wazalishaji zilionyesha makontena hayo yalikuwa na dhahabu tani 1.1 yenye thamani ya Sh97.5 bilioni.
Lakini Acacia katika moja taarifa zao za hivi karibuni juu ya ufafanuzi kuhusu makinikia wanaeleza kuwa kontena moja la tani 20 lina thamani ya wastani wa Sh310 milioni. Hii ina maana kuwa mzigo wote uliomo kwenye makontena 277 una thamani ya Sh85.87 bilioni.
Kwa hesabu za Acacia ambazo zinajumuisha madini ya dhahabu, fedha na shaba pekee, Serikali ilitakiwa kupata mrabaha wa Sh3.43 bilioni. Kampuni hiyo inapinga kuwa madini mengine yaliyosalia yaliyoorodheshwa na kamati hayana thamani ya kibiashara.