Unajua mnisamehe kidogo; kuna hisia mbaya sana ya uduni (acute sense of inferiority complex). Kwanza, tunaamini tutashindwa kama kes itatokea kati ya serikali na Acacia. Tutashindwa kwa sababu hatuwezi kushinda! Lakini kuna kitu kingine pia kinajionesha. Chukulia kwa mfano hoja ya "mikataba"; sote tunajua jinsi gani suala la mikataba mibovu limeisumbua nchi yetu na jinsi ambavyo ukweli kabisa upinzani ulifanya kazi kubwa sana kuonesha. Sasa unajiuliza; kama kuzuia makontena 277 tu tunaambiwa tutalizwa na tutalipishwa vibaya itakuwaje kama tukigusa mikataba?
Ndugu zetu katika woga wao wanasema "tusifanye lolote kwa sababu itatugharimu"; Wanasahau kuwa wakati mwingine mtu inabidi uchukue maamuzi ya kutetea maslahi yako hata kama itakuja gharama kubwa. Kuna watu wanaamua kuachana katika ndoa wakijua kabisa kuwa kwa kufanya hivyo (ni mkataba huo) watatakiwa kulipa gharama kubwa sana kwa yule mwingine. Lakini watafanyaje sasa? Abakie kwenye uhusiano ambao unahatarisha afya yake ya akili na mwili au atoke ili atafute ahueni kwingine hata kama kwa kufanya hivyo atatakiwa kulipa gharama ya matunzo kwa yule mwingine au atalazimika kugawana mali walizochuma pamoja? Kwa wengine, huo siyo uamuzi mgumu kivile.
Katika mahusiano ya biashara ya kimataifa hili pia si jambo geni; nchi, makampuni na hata watu binafsi wanaweza wakafika mahali wakaona kuwa hali iliyopo (status quo) haiwezi kuendelea na watatafuta namna ya kutatua tofauti zao lakini kama ikibidi wataenda mahakamani kutafuta judicial intervention (mahakama iingilie kati). Wanapofanya hivyo ina maana wanakuwa tayari kwa matokeo yoyote lakini hofu ya gharama peke yake haiwezi kuwa sababu ya kutokuchukua maamuzi yenye maslahi kwa upande husika.
NImewasoma ndugu zangu wengi wakitolea mfano wa mambo mbalimbali ambayo yamewahi kufanywa chini ya Magufuli na kuwa yamekuja kuligharimu taifa. Lakini kama ni gharama ya lazima kwanini tusilipe? Ni kweli kuna haja ya kuwa waangalifu; lakini uangalifu usije kugeuka kuwa woga! Jambo jingine la kuzingatia hapa ni kuwa katika sakata hili la makontena ya michanga mwenye maslahi makubwa ni taifa na siyo kampuni; hivyo kama taifa ni lazima tuangalie maslahi yetu lakini kama maslahi yetu yanatishiwa sana ni jukumu letu kuyatetea kwa umakini, weledi na uangalifu. Lakini kamwe tusisite kuyaangalia maslahi yetu kwa sababu tunaogopa wakubwa wanaweza kutushtaki au wanaweza kuamua kuondoa uwekezaji wao.
Mikataba hii ambayo tunasema "tuipitie" na tumeshadai kuwa ipelekwe Bungeni; lengo litakuwa ni nini? Je, tukiipitia au tukiipeleka Bungeni tutataka tuifumue tu tuifute au tuijadili upya? Vipi kama hao "wakubwa" wakigoma kupitiwa tena mikataba yao na wakikataa tusiiguse kwa sababu ni mikataba halali? Je, kama tukifanya hivyo kwa maamuzi yetu wenyewe (unilaterally) siyo kwamba watatupeleka kwenye arbitration ambako tutaweza kupoteza kama tulivyofanya kwenye Dowans? na kesi nyingine?
Wanaosema "tupitie mikataba" - jambo ambalo wengi tunalikubali na tumelipigia kelele miaka nenda rudi - hawajui kuwa wakubwa hawa kama kuna kitu watatubana nacho sana na hawako tayari kukiona ni kupitiwa mikataba hii. Sasa, Magufuli akiamua kusitisha mikataba na kuipitia yote (na ninatabiri hili itakapokuja ile kamati nyingine na matokeo yake) je, tutamuunga mkono au tutahamisha magoli tena na kusema "kwanini anaingilia mikataba halali!? hajui watatunyoa na mchanga!"?
Kwa sababu baada ya ile Kamati Magufuli anaweza kuleta usitiswhaji wa muda (Moratorioum) ya hata miezi sita ili kulipa taifa na wataalamu wake kupitia mikataba hiyo. Je, tutakubali na kuunga mkono au tutakimbia tena na kusema "mamaaa wee kagusa mikataba sasa, nchi itakimbiwa"?
Matokeo yake ni kana kwamba tunaambiwe kile alichoambiwa yule mwizi kwenye simulizi fulani 'ukisimama nchale, ukikimbia nchale, ukizungumza nchale, ukiguna nchale, usimeze, usiteme, wale usimumunye"! Ndio maana unaona kuwa Magufuli amefanya kile ambacho Wasambaa wanasema kama ni 'mbwai na iwe mbwai'!
Nawatakieni Mfungo Mwema wa Mwezi wa Ramadan.