Uamuzi wa Serikali kuhusu suala la usafirishaji wa mchanga wa madini, utategemea ripoti ya kamati ya pili iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza suala hilo.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Gerson Msigwa ikiwa ni siku moja baada ya kampuni ya Acacia kuitaka Serikali kuunda kamati huru kuchunguza kiasi cha madini kwenye makontena yake 277 yaliyozuiwa bandarini.
Wiki iliyopita, Rais Magufuli alikabidhiwa ripoti na kamati ya kwanza iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ambayo ilibaini kuwa makontena hayo yana tani 7.8 za dhahabu.
Pia, Acacia wanadai hawakupewa ripoti ya kamati hiyo licha ya kutoa ushirikiano wakati wa uchunguzi.
“Sijui chochote kuhusu hao Acacia kuomba iundwe kamati huru, lakini tunasubiri ripoti ya kamati ya pili iliyoundwa kuchunguza sakata hili wampelekee ripoti Rais,” alisema Msigwa.
Wakati Ikulu ikisema hayo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alizungumzia ripoti ya kamati ya Profesa Mruma na kusema chanzo cha hayo ni sheria mbovu za madini pamoja na mikataba iliyotungwa katika kipindi cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa. “Tanzania inaruhusu kupitishwa kwa sheria mbovu na wizi halafu baadaye wanapiga kelele, wapinzani tunasema sheria zote lazima zifumuliwe na kupangwa upya,” alisema.
Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai alionyesha shaka kuwa ni lazima Taifa litaingia kwenye migogoro mikubwa ya kidiplomasia kutokana na ukiukwaji wa sheria unaofanywa ikiwamo sakata la mchanga huo.
Alisema itachukua muda mrefu kwa wawekezaji kuiamini tena Tanzania na kuja kuwekeza kwa kuwa hata waliopo wameanza kuondoka.
Pia, Mbowe alisema kuna tetesi kuwa uchunguzi huo ambao ulimng’oa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo una upungufu mwingi.
Suala la fedha nalo limeibuka katika sakata hilo.
Akizungumzia suala hilo, aliyekuwa mjumbe wa Mpango wa Uhamasishaji wa Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (Teiti), Bubelwa Kaiza alisema ipo haja ya kupitiwa upya kwa taarifa za fedha za kampuni za madini ambazo zilikuwa zikiwasilishwa.
Kaiza alisema kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya kuchunguza mchanga wa madini iliyowasilishwa siku chache zilizopita ni wazi kampuni hizo hazikuwa zikitoa taarifa sahihi.
Alisema Teiti ilikuwa inapitia taarifa za fedha ambazo zilikuwa zinawasilishwa kwa hiari na kampuni husika na si kuchunguzwa, hivyo upo uwezekano walikuwa wanatumia mwanya huo kutoa taarifa za uongo.