Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye si wa kwanza kustaafu ukurugenzi wa bodi ya Benki ya CRDB. Ni utaratibu uliopo ndani ya taasisi hiyo ya fedha, kuchiana vijiti licha ya malipo manono yanayoambatana na nafasi hiyo.
Sumaye alitangaza kujiondoa kwenye bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo kwenye mkutano mkuu wa 22 uliofanyika jijini Arusha wiki iliyopita, jambo lililozusha mjadala miongoni mwa wadau wengi wa biashara hasa sekta ya fedha.
Kujiuzulu kwa Sumaye aliyedumu kwenye bodi hiyo tangu mwaka 2011, kulitoa nafasi ya kuchaguliwa kwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Neema Munisi.
Sumaye na mrithi wake, wamo kwenye kundi la wenye chini ya asilimia moja ya hisa zote za kampuni ambao wanatakiwa kuwa na mkurugenzi mmoja miongoni mwa 13 wanaotakiwa.
Kwenye mkutano huo, Dk Neema aliwashinda wenzake baada ya kupata asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa. Wanahisa zaidi ya milioni 527 walipiga kura kwenye uchaguzi huo.
Kuepusha mgongano wa maslahi, benki inawataka wakurugenzi wake kueleza bayana kama wanazo biashara zenye ushindani na CRDB. Ni sharti mkurugenzi kutokuwa na biashara au ajira ya kudumu yenye mgongano wa maslahi na benki hiyo.
Siasa zimemuondoa Sumaye, ambaye anasema atalazimika kutumia muda mwingi kuitumikia Chadema katika kujipanga na uchguzi mkuu ujao au wowote utakaojitokeza kabla ya mwaka 2020.
“Mambo yangu mengi yanafuatiliwa. Hata mashamba ya wanangu yamechukuliwa. Sitaki kuiingiza benki hii yenye maelfu ya wanahisa kwenye matatizo kwa ajili yangu,” anasema Sumaye.
Sumaye mwenye zaidi ya hisa milioni 7.448, amejiondoa kwenye bodi hiyo licha ya mamilioni ya shilingi aliyokuwa akilipwa kutokana majukumu aliyokuwa akitekeleza. Kumbukumbu za benki hiyo zinabainisha; mwaka jana alilipwa Sh58 milioni kati ya Sh616 milioni, wakati mwaka 2015 alipokea Sh53 milioni kati ya Sh553 milioni zilizotengwa kwa ajili ya malipo ya wajumbe wa bodi. Malipo hayo yalifanywa baada ya Sumaye kuhudhuria vikao saba kati ya vinane vilivyopangwa na kufanyika mwaka 2016.
Mwanasiasa huyo amejiondoa wakati bajeti ikiwa kwa ajili ya posho za wakurugenzi ikiwa imeongezeka. Zaidi ya Sh700 milioni zinatarajiwa kutumika kwa ajili hiyo mwaka huu.
“Hata baada ya uamuzi huu rafiki zangu wa Mtaa wa Lumumba hawafurahi. Nilitarajia wataridhika kwa kuona nitakosa posho hizi zinazolipwa kwa wajumbe,” anatania.
Waliiojiuzulu
Bodi ya wakurugenzi ndiyo mamlaka ya juu inayosimamia utawala ambayo inazo kamati zinazoshughulikia vihatarishi vya mikopo, ukaguzi, utawala na rasilimali watu ili kuongeza umadhubuti wa biashara na fedha.
Kwenye mkutano mkuu uliopita, wajumbe watatu; Boniface Muhegi, Ally Laay na Adam Mayingu walistaafu. Mayingu hakutaka kurudi tena, lakini Laay aligombea na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti baada ya kustaafu kwa Martin Mmari. Muhegi bado yupo kwenye bodi hiyo baada ya kuchaguliwa tena.
Bodi ya wakurugenzi wa CRDB ina wakurugenzi 13, miongoni mwao 12 siyo watendaji akiwamo mwenyekiti isipokuwa mkurugenzi mtendaji. Mwenyekiti huchaguliwa kila mwaka kuiongoza bodi hiyo.
Kila mwenye asilimia 10 ya hisa za benki huruhusiwa kuchagua mkurugenzi wa benki. Wenye kati ya asilimia moja mpaka 10 huruhusiwa kuchagua mkurugenzi kwa kila asilimia 10, wale ambao hawafikishi asilimia 10 kwa ujumla hawaruhusiwi kuchagua mkurugenzi.
Kwenye mkutano mkuu uliofanyika mwaka 2015, wanahisa walikubaliana kuwaruhusu International Finance Co-operation (IFC), Africa Capitalizationa Fund (AFCap) na Kampuni ya CDC (Commonwealth Development Corporation) Group kuteua mkurugenzi mmoja iwapo hisa zao zitafika asilimia tano.
Wanahisa wanaomiliki chini ya asilimia moja ya hisa zote, wanaruhusiwa kuchagua mkurugenzi mmoja na wanahisa wote kwa pamoja wanaweza kuchagua mkurugenzi huru.
Kwa mujibu wa katiba ya benki, wajumbe wa bodi wanapaswa kustaafu ingawa wanaweza kuchaguliwa tena baada ya muda wao wa miaka mitatu kumalizika iwapo wanakidhi vigezo.
Itakumbukwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi, Martin Mmari aliteuliwa na Mfuko wa Pensheni wa PPF na alistaafu tangu Julai 2016 na nafasi yake kujazwa na Hosea Kashimba.
Profesa Mohammed Warsame alichaguliwa kuwakilisha kundi la wenye hisa kati ya asilimia moja mpaka 10, wakati Madren Oluoch-Olunya alichaguliwa kuwa mjumbe huru akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Lawrence Mafuru.
Bodi ina jukumu la kusimamia na kupitisha malengo na mikakati ya benki na kampuni zake tanzu na kufuatilia utekelezaji, kusimamia utekelezaji wa mfumo wa utawala kuhakikisha unaendana na mabadiliko yoyote kama vile ukubwa, mtandao wa shughuli, mkakati wa biashara, masoko na udhibiti.
Vilevile, hushirikiana na menejimenti kuangalia vihatarishi na sheria za udhibiti zilizopo na maslahi ya muda mrefu ya kampuni kwa ufanisi.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk Mlenge Fanuel anasema kuondoka kwenye bodi ya wakurugenzi siyo kitu cha ajabu kwa wajumbe wa taasisi nyingi.
“Kitu muhimu ni ufanisi wa taasisi husika. Kama huduma zake zinakidhi matarajio ya wateja, hakuna tatizo lolote. Ni kawaida kwa wajumbe kupishana. Waikuwapo wengi CRDB ambao waiondoka,” anasema Dk Fanuel.
Credit - Mwananchi