Jambazi Mwanamke Mrembo Auawa na Polisi Nairobi

Mwanamke anayedaiwa kuwa jambazi sugu, ambaye amekuwa akipakia mtandaoni picha zake akiwa amejipodoa na kujipamba, ameuawa na polisi jijini Nairobi.

Kijana huyo ambaye ametambuliwa kama Claire Mwaniki aliuawa na polisi alfajiri na mapema Jumatano katika mtaa wa kayole.

Gazeti la kibinafsi la Daily Nation linasema mwanamke huyo alikuwa na majambazi wengine wane wa kiume pale walipofumaniwa na polisi wakitekeleza wizi katika eneo la Lower Chokaa, mtaa wa Kayole.

Anadaiwa kufyatulia risasi maafisa wa polisi akiwa na jambazi mwingine lakini wawili hao wakauawa.

Taarifa katika gazeti la Daily Nation inasema polisi waliwaandama baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wenzao kupitia WhatsApp kwamba majambazi hao walikuwa wamekwepa mtego waliokuwa wamewekewa.



Polisi walijiandaa na kisha wakawakabili katika mtaa wa Lower Chokaa.
Mkuu wa polisi wa mtaa wa Kayole Joseph Gichangi amenukuliwa na gazeti la Daily Nation akisema: "Kwa mujibu wa wadokezi wetu, mwanamke huyo alikuwa mke wa mshukiwa wa ujambazi ambaye anafahamika vyema, ambaye bado anasakwa na polisi."

Alisema visa vya wanawake kujihusisha na magenge yanayotekeleza wizi wa kutumia mabavu vinaongezeka.

Wakenya mtandaoni wamekuwa wakisambaza picha za Mwaniki na kumjadili sana mtandaoni.
Katika Facebook, mwanamke huyo anajitambulisha kama mwanafunzi wa zamani wa chuo kikuu cha Nairobi na mtu anayependa kufurahia maisha.

Kuna wakati alipakia picha yake, ya mwanamume na mtoto, na kuongeza kwamba hiyo ni "familia".
Mkuu wa polisi Nairobi Japheth Koome anasema magenge mengi ya wahalifu huwa na wanawake.

"Wanawake hutumiwa kusafirisha silaha, kukusanya habari na hata kushiriki katika ujambazi," Bw Koome alisema.

Aliongeza kuwa wakati mwingine hutumiwa na majambazi wa kiume kuwapelekea chakula mafichoni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad