Jeshi la Polisi Lawamani Tena..Lamuua Mwanafunzi Mwingine wa Chuo Kikuu kwa Kumpiga Risasi Nyumbani Kwao..!!!


Utata umeibuka kuhusu kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Uvuvi Mbegani, Boniventure Kimali (25) baada ya ndugu kudai ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi akituhumiwa kuwa jambazi.

Kimali aliyekuwa akihudhuria mafunzo kwa vitendo katika Soko la Samaki Feri akitarajiwa kuhitimu stashahada Juni mwaka huu katika fani ya uchakataji samaki, ubora na masoko inadaiwa aliuawa nyumbani kwao, CCM Shule eneo la Vijibweni.

Mwandishi wa habari hii aliyefika nyumbani hapo na kuonyeshwa eneo ambalo inadaiwa aliuawa kulikuwa na damu ukutani.

Pia, mwandishi alionyeshwa maganda ya risasi ambayo ndugu zake wameyahifadhi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, alielekeza atafutwe kaimu wake. “Mimi nipo nje ya ofisi mtafute kaimu wangu.”

Kaimu kamanda huyo, Nyigesa Wankyo hakupatikana kwa siku ya mkononi iliyoita bila kupokewa vivyo hivyo kwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro.

Naftani Balampame, ambaye ni kaka wa Kimali alisema tukio hilo lilitokea Ijumaa saa 3:30 usiku walipokuwa mbele ya nyumba yao, huku mdogo wake akiwa anafua.

“Tulikuwa tunazungumza hapa nje, yeye (marehemu) akawa amechukua simu yangu anazungumza, ghafla tukasikia milio ya risasi, sisi tulikimbilia ndani yeye alikimbia akielekea nyuma ya nyumba,” alisema Balampame.

Alifafanua kuwa walisikia milio ya risasi nyuma ya nyumba na baadaye walisikia sauti anazodai ni za askari wakisema “si yeye huyu” na mmoja wao alizungumza na simu kuita gari.

“Mdogo wangu aliniita akitaka nimpeleke hospitali, nilipojaribu kusogea walinifukuza, walimwingiza kwenye gari na kuondoka naye. Tulikwenda kituo cha polisi ambako walituambia amepelekwa Hospitali Kigamboni,” alisema.

Alisema walipokwenda hospitali walielezwa hawakumpokea kutokana na kukosa maelezo kumhusu na kwamba polisi Kigamboni waliwaeleza aliuawa kimakosa, kauli iliyobadilishwa baadaye.

Kaka mwingine wa marehemu, Daudi Gwelenza alisema katika Hospitali ya Taifa Muhimbili walipewa taarifa kwamba umepokewa mwili wa kijana asiyejulikana.

“Niliomba kuuona mwili nikamkuta ndiye yeye ana tundu la risasi tumboni na ana mchanga wa bahari. Maelezo yanaonyesha alifikishwa saa 10:00 alfajiri na askari Fatuma Abdallah ikielezwa amekufa kwa kipigo,” alisema Gwelenza.

Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti kutoka Chuo cha Uvuvi Mbegani kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, Ambakisye Simtoe alisema kifo hicho kimeushtua uongozi wa chuo kwa kuwa mwanafunzi huyo aliruhusiwa kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo wiki mbili zilizopita.

Msemaji wa familia hiyo, Goodluck Kimali alisema hawajui watazika lini wakisubiri polisi watoe tamko. “Kwetu ni Kigoma, tunatarajia wafanye uchunguzi ijulikane wazi nini msimamo wao na wetu, ili tuuchukue mwili tukazike nyumbani,” alisema.     

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad