JPM - Naomba Mniombee Ili Urais Usinipe Kiburi..Maisha Haya ni ya Mpito Tu..!!


RAIS John Magufuli maetoa ombi zito kwa viongozi wa dini nchini wakiwamo maaskofu baada ya kuwataka wamwombee ili kazi yake ya urais isimpe kiburi bali aendelee kuwa mtumishi mwema wa watu.

Rais Magufuli alitoa ombi hilo kwa nyakati tofauti jana wakati aliposhiriki ibada ya Jumapili kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Moshi Mjini na Kanisa Kuu la Kiaskofu la Parokia ya Kristo Mfalme (la katoliki), pia la Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.

Magufuli aliomba maaskofu na viongozi wengine wa dini wamuombee wakati akiwa katika kanisa la Usharika wa Moshi, kwenye ibada iliyoongozwa na Mkuu wa Kanisa la KKKT Tanzania, Askofu Dk. Fedrick Shoo na baadaye katika Kanisa la Kristo Mfalme ambako ibada iliongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Mhashamu Isaac Amani.

Awali, akiwa katika kanisa la KKKT, Askofu Shoo alimuomba Rais Magufuli kujitenga na washauri wanaojikomba na badala yake apokee ushauri unaotolewa na washauri wema na wenye nia njema kwake na kwa taifa.

“Tunamuomba Mungu akupe washauri wazuri wasio na hila na wasiojikomba kwako….na ambao hawatakuwa na ajenda za kujinufaisha binafsi. Pale unapoona mambo hayaendi na umepungukiwa, sisi kama kanisa na Watanzania wenye nia njema tunasema tupo tayari kukushauri na kukuombea,”alisema Askofu huyo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini.

Aidha, Askofu Shoo alisema pamoja na jitihada mbalimbali za maendeleo zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya tano, bado kumekuwa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiona mabaya tofauti na yale mazuri ambayo yamekuwa yakifanywa na serikali, jambo ambalo sio sahihi.

“Tunamuomba Mungu atupe Watanzania ambao wana uwezo wa kuona mema ambayo umekuwa ukiyatenda  na umekuwa ukiyafanya katika kipindi hiki kifupi cha utawala wako,” alisema Dk. Shoo

Dk. Shoo aliongeza kuwa kanisa lake litaendelea kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali katika utumbuaji majipu na kuwashughulikia wale wote ambao wamekuwa wakiishi kwa kutegemea shughuli za magendo na rushwa.

Alimwomba pia Rais Magufuli kuangalia uwezekano wa kuzipunguzia taasisi za dini mzigo wa kodi ambazo wanatozwa pale wanapoingiza mali ambazo zimekuwa zikitumika kutoa huduma za kijamii.

Wakati alipoitwa na Dk. Shoo ili kutoa salamu kwa waumini wa kanisa hilo, ndipo Rais Magufuli alipoomba viongozi wa dini wamuombee ili madaraka aliyo nayo yasimpe kiburi.

Alisema mtu anaweza akapata madaraka na kuwa kiburi, na akafanya mambo ya ajabu wakati maisha yenyewe ni ya temporary (muda), jambo ambalo yeye anaomba lisimtokee.

“Mheshimiwa Baba Askofu, ombi lako kuhusu kodi kwa taasisi za dini nitalibeba na nitalifanyia kazi. Haiwezekani mtu unaagiza X - Ray machine kwa ajili ya huduma halafu ulipe kodi. Nitazungumza na viongozi wa Wizara ya Fedha wajadili na kuona namna ya kulishughulikia,”alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alilichangia kanisa hilo (KKKT) mifuko 150 ya saruji kwa ajili ya shughuli za ujenzi na pia kuizawadia kwaya ya Usharika wa Moshi Mjini Sh. milioni moja.

IBADA KANISA KRISTO MFALME

Katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Parokia ya Kristo Mfalme, Askofu Amani alisema ni vyema wananchi wakaendelea kulinda amani na umoja wa taifa kwani ni dhahiri kuwa amani iliyopo inalindwa pia na wananchi na siyo majeshi peke yake kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.

Baada ya kumaliza mahubiri yake, Askofu Amani alimpa nafasi Rais Magufuli kutoa salamu zake ambapo alisema: “Najua urais mnao ninyi na mliamua niwe mtumishi wa watu. Naomba muendelee kuniweka kwenye maombi ili kazi hii ya urais isinipe kiburi… niwe mtumishi wa watu.”

Akieleza zaidi, Rais Magufuli alisema amekuwa mtu wa kufikiriwa vibaya  na baadhi ya watu kwamba ni mtu mkali, lakini ukweli ni kwamba yeye ni mkali kwa watu wanaofanya maovu.

Alisema ni vyema Watanzania wakaendelea kumuombea ili asiwe na kiburi cha madaraka na kuendelea kutekeleza kazi aliyopewa na Mungu na kwamba, amekuwa akifanya mabadiliko makubwa kutokana na ukweli kwamba nchi ilikuwa inaelekea pabaya.

Rais Magufuli alichangia pia Kanisa la Kristo Mfalme mifuko 100 ya saruji pamoja na kwaya ya kanisa hilo kiasi cha Sh. milioni moja.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad