"Kuna taarifa zinasambazwa kuwa mimi na viongozi waandamizi wa chama eti tulivamiwa na wanachama na kufukuzwa Tanga Mjini kwenye Ziara.
Ukweli ni kuwa ziara ile ya juzi Jumapili ilizuiliwa na Polisi siku hiyo hiyo kama mwendelezo wa hujuma ambazo tunafanyiwa na Wasaliti (Lipumba na Wenzake) wakishirikiana na Vyombo vya Dola.
Mapokezi niliyopewa Tanga yalikuwa makubwa mno na tulifanikiwa kufanya kikao kimoja cha ndani (Na Kamati ya Utendaji ya Wilaya, Madiwani na Wabunge) - Wakati kikao kinaendelea magari ya Polisi yalikuja kuzingira Ofisi ya Wilaya na kututaka tusitishe kikao hicho.
Niliwasihi viongozi wakubaliane na amri hiyo ya Polisi ili kuepusha shari na mapambano yasiyo na tija wala faida kwa chama na kwa usalama wa kila mmoja.
Nje ya Ofisi ya Wilaya kulijaa mamia ya wanachama wa CUF ambao nao walitaka niwahutubie, nilishindwa kupata wasaa huo kwa sababu Polisi walisema tutekeleze amri yao.
Siku moja kabla ya mimi kufika Tanga Polisi walitoa barua ya kuruhusu ziara yangu, ila siku ya ziara yenyewe walipokea maelekezo kutoka ngazi za juu kuwa waisitishe kwa hiyo wakakabidhi barua ya sitisho muda uleule wakati vikao vikiendelea (siku ya ziara).
Na mwisho, Tanga iko shwari sana. Kijikundi cha Lipumba kimejichimbia Buguruni tu, huko mikoani kuko shwari sana na hawawezi kukanyaga wala kutisha watu. Dar Es Salaam kwenyewe kikundi hicho kina ngome kwenye maeneo machache sana ambayo pia yanazidi kumomonyoka.
Hata hivyo, kama kungekuwa na kijikundi kimekuja kutuvamia Tanga, ningeliamrisha mamia ya wanachama wa CUF waliokuwepo wakishughulikie na tayari tumeshawaelekeza wanachama wetu hasa mkoani Dar Es Salaam, wakivamiwa na vikundi vya wahuni (kwa mfano ule wa Hotel ya Vina - Mabibo) basi wajilinde kwa nguvu zote, wavidhibiti vikundi hivyo na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola."
Mtatiro J,