Kamati ya Mashehe Mkoa wa Mwanza, wiki iliyopita ilimsimamisha huduma Shehe Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Ahmad Ally Jaha ambaye pia ni mfanyakazi ‘mtingaji’ wa Mgodi wa Geita Gold Mine ‘GGM’ kwa madai ya kukutwa na picha kwenye simu yake ya mkononi akiwa anabadilishana mate ‘denda’ na mwanamke ambaye si mke wake.
ALIYENASA PICHA HIZO
Tukio hilo lilijiri hivi karibuni baada ya mke mkubwa wa Shehe Jaha kubaini uwepo wa picha za mumewe na mwanamke mwingine ‘mchepuko’ wakila denda, jambo lililomkasirisha na kumsikitisha kwa kuwa, mumewe ni kiongozi wa dini na hakustahili kufanya hivyo kulingana na maandiko.
MTIRIRIKO WA TUKIO
“Ni kweli Shehe Jaha amesimamishwa baada ya mkewe kukuta picha chafu za mwanamke mwingine na mumewe wakiwa wanakula denda.
“Kimsingi mkewe alikasirika sana na kuamua kwenda kutoa malalamiko yake kwenye ngazi husika.
“Yale malalamiko yalitua kwenye Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Sengerema na wao kutokana na uzito wake, wakayawasilisha kwenye ngazi ya juu kabisa, yaani taifa.
“Inasemekana kwamba, mwanamke aliyenaswa kwenye picha na Shehe Jaha ndiye anayeishi naye kule kazini kwake, mgodini Geita ambaye kimsingi ni mchepuko,” kilidai chanzo chetu.
SHEHE ANA WAKE WATATU!!
“Kinachonishangaza, inadaiwa Shehe Jaha ana wake watatu, lakini aliyenaswa naye kwenye picha si miongoni mwa hao wake zake watatu.
“Kwa hiyo wake watatu mbali, huyo ni mchepuko wake. Hivi unadhani hata kama ni wewe ungefanyaje?” kilihoji chanzo chetu ndani ya Bakwata wilayani Sengerema.
KATIBU WA BAKWATA
Akizungumza na Wikienda baada ya tukio hilo la aina yake, Katibu wa Wilaya ya Sengerema, Shehe Madaraka Zubery, alithibitisha kusimamishwa kwa Shehe Jaha kwa kupewa barua iliyotolewa kutokana na maamuzi ya uongozi wa juu wa Bakwata Mkoa wa Mwanza.
Kwa mujibu wa katibu huyo, maamuzi hayo yaliidhinishwa na Shehe Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Salum Fereji kutokana na Jaha kukiuka misingi na maadili ya Kiislam na kutumia vibaya madaraka yake na kuwatia aibu Waislam.
Hivyo, alisema kuwa, kamati hiyo ilimteua Shehe Hassan Nuhu kukaimu nafasi yake hadi pale taarifa rasmi itakapotamkwa na Makao Makuu ya Bakwata Taifa jijini Dar es Salaam kama anastahili kuondolewa kabisa au lah.
MTUHUMIWA HUYU HAPA
Baada ya kumsikia Shehe Zubery, Wikienda lilimtafuta Shehe Jaha anayetuhumiwa na alipopatikana alielezwa kila kitu kuhusu sakata hilo kuanzia kusimamishwa huduma, kuwa na wake watatu na madai ya kuishi na mchepuko mgodini, Geita.
Hata hivyo, katika kujibu madai hayo, Shehe Jaha alionesha kushtushwa zaidi na taarifa za kusimamishwa kuliko maswali mengine kwani alionesha kama mtu ambaye alikuwa hajui kinachoendelea kisha akasema yeye hana taarifa kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi yake.
Alisisitiza kuwa, hajui kama amechukuliwa hatua ya kusimamishwa huduma hivyo anaendelea na kazi zake kama kawaida hadi atakapojulishwa rasmi kwa maandishi.
“Sina hizo taarifa, sijui kama nimechukuliwa hatua na mimi naendelea na kazi zangu kama kawaida, sijapewa barua rasmi, nasikia tu kwa watu,” alisema Shehe Jaha kisha akakata simu bila kufafanua mengine.