Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ameitaka Serikali kuacha kutumia michango inayotolewa kwa wahanga wa majanga, kwa matumizi yake.
Sumaye, ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza kushika nafasi hiyo kwa miaka kumi mfululizo, alisema hayo akitoa mfano kwa wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera pamoja na ajali iliyoua watu 35 wa Shule ya Lucky Vicent ya jijini Arusha Mei 6.
Fedha za misaada ya wahanga wa tetemeko la ardhi, takriban Sh7.5 bilioni zilitumiwa kukarabati miundombinu iliyoharibika, wakati za ajali ya basi la Lucky Vicent zimetumika kwa shughuli mbalimbali za kuaga maiti na mazishi na hivyo kuibua lawama kuwa baadhi ya matumizi hayakutakiwa kugharimiwa na fedha hizo.
Ajali ya Lucky Vicent iliua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja. wanafunzi watatu walionusurika, wamesafirishwa kwa msaada kwenda Marekani kwa matibabu zaidi, wakiwa pamoja na daktari, muuguzi na mzazi mmoja kila mwanafunzi.
“Tujuavyo, huwa tunachangia kuwasaidia waliopatwa na tatizo. Huu utaratibu mpya wa kuichangia Serikali kupitia misiba au majanga umeanza lini na ni chombo gani kimeupitisha?” alihoji Sumaye.
Kutokana na matukio hayo mawili na kilichofanywa na Serikali, Sumaye alisema utaratibu huo si sahihi kwa sababu unawadhulumu wale waliotakiwa kusaidiwa na kuwavunja moyo wachangiaji.
“Ni aibu kubwa sana kwa Serikali kufanya hivyo. Serikali iache kutumia mabavu kuchukua michango ya watu na kuitumia kinyume na watoaji walivyodhamiria,” alisema.
Licha ya mabadiliko ya matumizi yaliyofanywa katika rambirambi, mkuu wa mkoa wa Arusha aliagiza kukamatwa kwa watu waliojitokeza kwenda kutoa pole zao katika shule hiyo na kuzuia Sh18 milioni walizotaka kuikabidhi Lucky Vicent.
“Watanzania wapenda amani na wapenda haki lazima tulaani kwa nguvu zetu zote kitendo hicho cha uonevu, ukatili na uvunjifu wa haki za binadamu,” alisema Sumaye.
“Mtindo wa kutesa watu wasio na hatia kwa sababu za kisiasa ni chachu ya machafuko katika nchi na amani hii tuliyonayo ikitoweka, hakuna atakayepona.”