DAR ES SALAAM: Baadhi ya wazazi wenye watoto wanaosoma shule za jijini Dar zinazotumia magari maalum ya kuwapeleka watoto shule (School Bus) wamejikuta wakihenyeka kufuatia magari mengi kuzuiwa kufanya shughuli zao kutokana na kuwa na matatizo mbalimbali. Mengi ya magari hayo yamepigwa ‘stop’ baada ya kutokea kwa ile ajali kule Arusha, wilayani Karatu iliyosababisha vifo vya watu 35 wakiwemo wanafunzi 32 kisha kubainika kuwa, gari walilokuwa wamepanda halikuwa na sifa za kufanya safari.
Kufuatia ajali hiyo, katika Jiji la Dar magari mengi mabovu yaliyokuwa yakisafirisha wanafunzi yamekuwa yakikamatwa, hali iliyosababisha wazazi na walezi wengi kuchukua jukumu la kuwapeleka watoto wao shule na kuwarudisha nyumbani. Amani juzi kwa nyakati tofauti lilishuhudia baadhi ya wazazi wakitembea umbali mrefu wakiwa na watoto wao na wengine kutumia usafiri wa daladala, Bajaj na bodaboda kuhakikisha watoto wao wanakwenda kupata elimu wakati siku za nyuma walikuwa wakitumia magari maalum.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina la mama Sonia wa Sinza jijini Dar alisema, yeye alikuwa akitumia School Bus ya kampuni binafsi lakini hivi karibuni alitumiwa meseji kuwa, magari yao yamekamatwa hivyo wanasitisha huduma kwa muda. “Kwa kweli nahenyeka sana na huyu mwanangu, naamka saa 11 asubuhi, napanda gari hadi Faya, nashuka kisha naanza kutembea hadi Shule ya Msingi Olympio, kila siku na jioni naenda kumfuata.
“Na hili siyo mimi tu, wazazi wengi wanakiona cha mtemakuni, imebainika magari mengi yanayobeba wanafunzi ni mabovu na hicho ndicho kinaleta hili tatizo. Wenyewe tulizoea asubuhi mwanao anapitiwa nyumbani, anapelekwa na kurudishwa, sasa hivi baadhi ya wazazi ndiyo wanafanya kazi hiyo,” alisema mzazi huyo.
Kuhusiana na hilo la kukamatwa kwa magari mengi yanayosafirisha wanafunzi, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, DCP Mohammed Mpinga aliliambia Amani kuwa, ni kweli polisi wamekuwa wakikagua
magari yote yakiwemo hayo ya wanafunzi ili kuhakikisha usalama kwa wanaotumia. “Nisisitize; Siyo mabasi tu, ni magari yote tunakagua. Nawaomba wote wanaoona magari yao hayafai kuwa barabarani kwa ubovu, wasingoje kukamatwa, watii sheria bila shuruti kwa kutoyaingiza barabarani,” alisisitiza Kamanda Mpinga.