Rufiji. Kuongezeka kwa mauaji ya viongozi wa serikali za mtaa na polisi kumeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kiuchumi, kisiasa na kijamii katika maeneo kadhaa wilayani Rufiji na Kibiti mkoani Pwani.
Awali, hali haikuwa mbaya lakini baada ya mauaji ya askari wanane Aprili, shunguli nyingi za kiuchumi na kijamii zilianza kuathirika baada ya vyombo vya ulinzi na usalama kuamua kutumia nguvu kubwa.
Hali hiyo imejenga hofu na sintofahamu miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo.Biashara nyingi zimefungwa na wananchi wengi hawaendi mashambani wakihofia, ama kukutana na wauaji au polisi wanaokuwa katika doria, ambao hawana ‘msalie mtume’ wanapomshuku mtu yeyote.
Na katazo la wananchi kutembea baada ya saa 12:00 jioni limezidisha hofu na limeondoa nafasi za vijana na kina mama wengi kufanya shughuli za kujiongezea kipato.
Hadi sasa zaidi ya viongozi 15. polisi 10, wafanyakazi wawili wa Idara ya Maliasili, mwananchi mmoja na watu wengine watatu waliokuwa wamevalia nguo za kike, wameshauawa tangu Mei mwaka jana. Na tangu mapema 2015, zaidi ya viongozi 21 wameshauawa.
Shughuli za serikali za vijiji zasimama
Pamoja na polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuweka kambi maeneo hayo, sehemu kubwa ya wilaya hizo ni kama hazina uongozi.
Viongozi wengi
Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu Mpakani wilayani Kibiti, Ramadhani Msanga aliyekimbilia mafichoni tangu Februari 4 baada ya nyumba yake kuchomwa na watu wenye silaha, ni kielelezo cha maisha ya hofu.
Dada wa mwenyekiti huyo, Shela Msanga anasema awali, kaka yake alikuwa akipata vitisho vya maneno na maandishi, lakini Februari 4 wauaji waliamfuata nyumbani kwake saa moja jioni wakiwa na bunduki.
“Kwa bahati kaka hakuwepo nyumbani,” anasema dada huyo.
Baada ya kumkosa, wauaji hao waliwaamuru wapangaji watoke ndani na baada ya kufanya hivyo, waliichoma nyumba hiyo moto.
Diwani wa Mjawa, Ramadhani Chepa anasema wenyeviti wa vijiji vyote saba wametorokea mafichoni na shughuli za Serikali zimesimama.
“Huduma zote za Serikali za mitaa zimesimama kwa sababu vikao vya maendeleo ya kata havifanyiki,” anasema Chepa.
Diwani huyo anasema ofisi ya Serikali ya kijiji hicho haijafunguliwa kwa miezi mitatu.
Ofisa mtendaji wa Kata ya Umwe wilayani Rufiji, Adam Mkumbaamani, pia amekimbia makazi baada ya kupata vitisho vya kuuawa mara mbili.
“Tishio la kwanza lilikuwa Aprili 2, 2017. Walikuja watu wawili kati ya saa tano na saa saba mchana. Walimkuta mke wangu mkubwa akawaambia sipo. Nilikuwa kwa mke mdogo, nikajiuliza kama ni watu wema kwa nini wasije ofisini,” alisema Mkumbaamani aliyezungumza na Mwananchi akiwa mafichoni.
“Aprili 15, 2017 walikuja tena usiku tukiwa tumelala, wakagonga mlango nusura ya kuuvunja. Kumbe wanafuatilia sana, maana gari yangu niliilaza kwingine tofauti na nilipolala, lakini wakajua. Nilitoa taarifa kitengo maalumu cha polisi.”
Mahudhurio shuleni yashuka
Hofu hiyo haijaathiri ofisi za Serikali za mitaa pekee. Shule nazo zimepata pigo.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) wilayani Kibiti, Hamza Malwile anasema wanafunzi wa shule za msingi za Jaribu na Uponda zilizopo katika Kata ya Mjawa, wamekimbia pamoja na wazazi wao.
Anasema hali hiyo imesababisha mahudhurio mabovu katika shule hizo ambazo zipo katika eneo ambalo askari tisa waliuawa baada ya kushambuliwa, akiwamo aliyekuwa ofisa upelelezi wa Wilaya ya Kibiti, Peter Kubezya.
Anasema baada ya kumalizika kwa likizo fupi, ni wanafunzi 46 tu kati ya 2,487 wa Shule ya Jaribu walioripoti shuleni, wakati Uponda yenye wanafunzi zaidi ya 1,000, ilipata wanafunzi wasiozidi 150 siku hiyo.
Lakini hali hiyo pia imewakumba walimu ambao wametoweka kutokana na kile wanachodai kuwa ni polisi kunyanyasa wananchi na watumishi wa umma.
“Serikali iangalie namna ya kuondoa changamoto hiyo kwa kukaa pamoja na wananchi wa maeneo haya ili warejee,” alisema Malwile.
Hali hiyo inathibitishwa na Mratibu wa Elimu wa Kata ya Mjawa, Sylvester Mbata.
“Baada ya kuuawa wale askari, hali haikuwa mbaya sana kwa walimu na wanafunzi kwa kuwa waliendelea kuhudhuria na kufundisha. Lakini ujumbe ulioachwa na wauaji baada ya jaribio la kuchoma kigango cha Kanisa Katoliki, umeongeza hofu kwa watumishi,” anasema Mbata.
Wahalifu hao waliacha ujumbe unaosomeka: “Tunatoa tahadhari, mmewaua ndugu zetu wawili siku ya Jumamosi na sisi leo tunaanza kazi kuanzia ngazi ya vijiji, kata na hata wilaya. Walimu madaktari, manesi watendaji wa vijiji na kata na taasisi zote.”
Malwile alisema walimu wamekuwa wakitaka ushauri wafanye nini kuchukua tahadhari.
Afya
Hofu hiyo pia imeathiri huduma za afya. “Huduma ya zahanaji inapatikana, lakini mganga mfawidhi ameshaomba kuhama kwa sababu ametishiwa kuuawa,” anasema Chepa, ambaye ni Diwani wa Mjawa.
“Zamani alikuwa anaishi hapa kijijini lakini sasa ameondoka kwa hiyo huduma ya saa 24 hazipatikani tena.”
Alipotafutwa katika zahanati hiyo, daktari huyo, Abdallah Mbonde alikataa kuzungumzia vitisho hivyo akisema taarifa zake ameshazipeleka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kibiti na katibu wa Idara ya Afya wa wilaya.
Diwani Chepa alisema kwa sasa wanategemea ulinzi wa Jeshi la Polisi na kikosi maalumu cha ulinzi kilichoweka kambi Kijiji cha Bungu.
Lakini Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rufiji, Rashidi Salum alisema kazi zinaendelea kama kawaida.
“Unajua hili ni suala tete sana, lakini sisi kama Serikali hatuwezi kusema tumeshindwa. Watumishi na wananchi kwa ujumla wanaishi kwa wasiwasi kwa usalama wao. Kwa kiasi fulani kuna athari ya ufanyaji kazi hasa maeneo ya vijijini, wananchi wanahofia kufanya shughuli zao, wafanyabiashara wana hofu, lakini wanaendelea hivyohivyo,” alisema Salum.
Lakini akasema Serikali imeongeza ulinzi katika ofisi za Serikali.
“Ungegeuka tu ukaona hata hii ofisi yangu inavyolindwa utakubali. Kwa hiyo shughuli hazijasimama, zinafanyika kwa tahadhari.
Kauli yake inalingana na ya Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari ya Ikwiriri, Said Omar aliyesema mahudhurio hayajaathirika.
Biashara zaaathirika
Sekta ya biashara nayo imeathiriwa na hofu hiyo. Moja ya makundi yaliyoathirika, ni ya wafanyabiashara wadogo waliokuwa wakifanya shughuli zao usiku au kukesha.
Kabla ha hali kubadilika, Amina Salum, mama lishe wa Ikwiriri, aliuza hadi kilo tatu za mchele.
“Biashara yetu ilikuwa inaanza saa 12:00 jioni, lakini hatuwezi tena,” alisema Amina aliyekuwa akitegemea madereva wa malori yanayotoka Kiwanda cha Saruji cha Dangote.
Hata shughuli za shamba sasa hazifanyiki.
“Utakwendaje shamba wakati kuna vitisho vya kuuawa? Tunasikia wanafanyia mazoezi porini, kwa hiyo unaweza kukutana nao,” anasema Juma Msati, mkulima anayeishi Kijiji cha Mpalage.