MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), ameeleza bungeni kile alichokiita ujumbe wa mwisho wa Ben Saanane, Msaidizi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
Akichangia mjadala wa makadirio ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Lema alisema: “Kama itanyesha mvua ya radi basi itaambatana na mwanga na cheche zitazowamulika walaghai, watesaji na watetezi wa haki watapata mwanga katikati ya giza totoro la unyanyasaji.”
Mbunge huyo alisema maneno hayo ni ujumbe wa mwisho ya Ben Saanane ambaye hajui kama ni marehemu ama yupo hai.
“Lakini hata kumjadili humu haturuhusiwi. Nje mikutano ya hadhara hatufanyi. Kama kijana wa miaka 16 katika Taifa ambalo halina uhuru wa vyombo vya habari, halina chama cha siasa aliandika maneno machache tu “Assad must go, Assad will be next, leo Syria haina amani,”alisema.
“Uhuru wa habari ni altenative (mbadala) ya amani, si kikwazo cha amani. Watu wanapoongea wanatema nyongo, ‘wanarealise tension’. Leo tunapotaka kujadili mambo ya msingi, mnatumia nguvu na uwezo mlio nao, mtashinda,” alisema Lema.
Alisema kila jambo wanalotaka kulipitisha kwa wingi wao watashinda.
“Katika mchango wangu uliopita, nilisema Mungu hadhihakiwi, apandacho mtu ndicho avunacho,”alisema
Alifunguka kuwa alipokuwa gerezani, vijana waliokamatwa kwa makosa ya mtandaoni ni wengi na walikamatwa kimya kimya.
“Wanapelekwa mahakamani wanasomewa mashitaka bila ndugu zao kuwapo. Vijana wamejaa magerezani kwa sababu ya ukosoaji,” alisema na kuongeza kuwa haiwezekani kuwa na taifa lenye amani bila kuwa na uhuru wa habari.
“Msifikiri mnatunga sheria kutukomoa sisi. Mna watoto wanakua, wajukuu wanakua…Tunapopigania uhuru wa habari hatupiganii Chadema, CCM tunapigania taifa bora na huru,” alisema.
“Leo ndani ya bunge hatusemi, kwenye mitandao hawaongei, vyombo vya habari havitasema huko mitaani mikutano ya hadhara imezuiwa. Iko siku watu wataingia mitaani kudai uhuru mnaowanyima.
Alisema watu hao watakuwa hawajatumwa na Chadema wala CUF na siku hiyo kila mtu atatafuta nyumba ya kujificha.
“Unapozuia haki, unapozuia uhuru, unapozuia kweli unatengeneza balaa katika taifa hili. Tunalalamika kwa sababu familia zetu zinaishi hapa, tungekuwa na mpango wa kuondoka tungeenda kulalamikia Marekani.
“Tukisema miongozo ni mingi na sijui hata hotuba yangu itakuwaje. Kama hotuba ya Waziri wa habari na michezo mmeifanya hivi, hotuba ya waziri wa mambo ya ndani na uzoefu wa Lijualikani alipokuwa magereza na uzoefu wangu nilipokuwa magereza mtaanza kuizuia kwenye salamu.
“Wabunge mko wengi tusaidieni, mawaziri tusaidieni tukishamalizwa sisi, msumeno utakaouata utakuwa kwenu. Ni nini mnakipigania waheshimiwa wabunge, kita kitu kinakuwa hovyo. Ni fedha?,” alihoji.
Lema alisema utu wa mtu haupimwi kwa ghorofa, cheo, bali unapimwa kwa kazi na wajibu alioufanya duniani.
“Mimi nilikamatwa nje hapo getini nikapelekwa Kondoa nikaweka ‘lock up’ (rumande) saa 4:00 hadi saa 8 usiku nikapelekwa Arusha nikatengwa chumba peke yangu, nikakaa jela nikatoka baada ya miezi minne. Mnaweza kufanya hivi leo,” alisema.
Lema aliongeza kuwa: “Mimi mkitaka kuniua niueni leo, kesho ni mbali. Mkitaka kumuua yeyote hapa muueni leo, kesho ni mbali. Haya mambo mnayotuzuia kuyasema mnafikiri tunasema tunapenda uwanaharakati.”
Alieleza kuwa ana mtoto wa kwanza ana miaka 11 na wa mwisho ana miaka minne na angependa kuona ndoa na harusi na elimu za watoto wake kwa macho yake.
“Lakini ikibidi nisione hiyo harusi kwa sababu ya kupigania ya ninachokipigania watakumbuka maisha yetu bungeni kupigania property (mali). Yalipigania haki na msingi wa taifa hili ambayo mmeishindwa,” alisema.
Alisema ni muhimu wanaokalia Kiti cha Spika wakaacha faraja, baraka na kuacha kutumia wingi wa wabunge wa CCM.
“Hapo alikaa Mzee Sitta leo ni marehemu, kila mtu atapita kwa wakati wake. Ni muhimu mkapita mkaacha faraja nyuma, baraka acheni kutumia wingi wenu vibaya. Simbachawene wewe una historia. Ulikuwa kondakta Mungu amekuweka mpaka umekuwa hapo, tulitarajia kukuona wewe unapigania nchi hii.
“Leo unaishi utafikiri umezaliwa katika familia ya Warren Bafet. Mtu akisimama kuongea ukweli unapinga.