MAALIM Seif Afunguka Jinsi Anavyoogopa Kuchukua Pensheni Yake ya Umakamu wa Urais..Adai Huwa Anajikimu kwa Pesa Zake za Mfukoni..!!!


KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad amesema kamwe hatumii fedha za serikali katika shughuli zake zozote ziwe binafsi au za kichama.

Alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa pia hatumii fedha yoyote ya Serikali kwenye matibabu yake.

Maalim Seif ameyasema hayo alipokuwa kwenye mahojiano ndani ya kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha runinga cha Couds Tv.

Maalim ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Zanzibar, alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa kama amekuwa akitumia fedha za Serikali katika shughuli zake mbalimbali.

Alisema Rais Dk. John Magufuli alipotoshwa kuwa Rais wa SMZ, Dk. Ali Mohamed Shein aliidhinisha fedha za matibabu za Maalimu Seif licha ya kukataa kumpa mkono.

Rais Magufuli alifanya ziara visiwani Zanzibar Septemba mwaka jana, ambapo alionesha kushangazwa na hatua ya Rais wa Zanzibar, kuidhinisha fedha za matibabu ya mpinzani wake wa kisiasa, Maalim Seif na kuongeza kuwa angelikuwa yeye kamwe asingeidhinisha.

Tukio hilo la Maalim Seif kukataa kumpa mkono Dk. Shein lilijitokeza Agosti mwaka jana wakati wa maziko ya Rais wa pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi yaliyofanyika makaburi ya Migombani.

Katika mazungumzo yake jana Maalim Seif alisema, alifanya makusudi kutompa mkono Dk. Shein ili kudhihirisha kuwa ndiye aliyempora haki yake.

“Kwanza Magufuli alipotoshwa kabisakabisa… tangu niache nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, nimekuwa nikijihudumia mwenyewe kwenye kila kitu,  si hela ya Makamu wa Rais ambayo nina haki ya kisheria kuipata. Lakini kwa sababu nawajua hawa ukiwaomba watakupa ila watakushambulia, watasema anachukua pesa zetu na hatutambui, kwa kweli najibana kwa njia yoyote ili kujihudumia. Kwa hiyo Magufuli alipotoshwa hakuambiwa ukweli, mimi hawanijui hawa,” alisema.

Alisema baada ya chama chao kutopatiwa ruzuku wameandaa utaratibu maalumu wa kupata fedha ambapo kila kiongozi wa ngazi ya kitaifa huchangia Sh 10,000 kwa mwezi, kiongozi wa ngazi ya wilaya Sh 3,000, Jimbo Sh 2,000 na mwanachama wa kawaida Sh 1,000 kwa mwezi.

“CUF msifanye mchezo nayo, tumewaambia wanachama kuwa huko nyuma hatukua na ruzuku, wakasema lazima tuchangie, na tumeweka utaratibu wa kuchangia. Tunajua hatuna wanachama matajiri kwa sababu  matajiri wanaogopa kuja CUF maana wakijulikana TRA watawatia adabu.” alisema

Alisema CUF kwa upande wa Zanzibar ina wanachama zaidi ya 200,000  kati ya wanzanzibar milioni 1.3 wakati Bara kinawachama milioni 1.5.

Aidha, alisema licha ya kwamba analipa kodi lakini haridhiki na serikali  iliyopo madarakani kwa namna inavyofanya kazi.

“Nalipa kodi shingo upande, lakini si kwamba naitambua serikali. Hata mkono sikumpa kwenye Msiba wa Abood Jumbe, nilifanya makusudi, kwani huyu ndiye aliepora haki yangu, ningempa wananchi wanione namchekea wananchi watanielewa vipi? nilikataa kumpa mkono makusudi ili ajue kuwa sikuridhika,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad