WAKATI zaidi ya watumishi 9,000 wakisimamishwa kazi mwanzoni mwa wiki hii, baada ya kukutwa na vyeti bandia, uchunguzi umebaini kuwa Serikali haijakubali kuwalipa mafao yao.
Taarifa za serikalini, zimesema katika mjadala wa namna ya kumalizana na watumishi hao kibinadamu unaoendelea, Serikali imeng’ang’ania, kuwa imewasamehe kupelekwa mahakamani.
Kwa mujibu wa sheria, watumishi hao wangepelekwa mahakamani, wangeshitakiwa kwa kosa la jinai na adhabu yao ni pamoja na kifungo cha miaka hadi saba jela.
Chanzo chetu cha uhakika kutoka karibu na mazungumzo hayo, kilibainisha kuwa mjadala huo umegawanyika pande mbili, mmoja ukitaka wafanyakazi hao wapewe mafao yao, kwa kuwa walitumia nguvu na maarifa kutumikia Serikali.
Upande huo unaosisitiza mafao yalipwe, imeelezwa kuwa umekuwa ukidai kuwa baadhi ya waliotajwa kuwa na vyeti hivyo walishastaafu wakisubiri mafao huku wengine wakiwa na hundi za malipo ya stahiki zao, lakini zimezuiwa mpaka Serikali itakapotoa kibali.
Katika kujenga hoja kwa mujibu wa chanzo hicho ndani ya Serikali, upande huo unaotaka mafao yalipwe, ulidai kuwa baadhi walikuwa kwenye likizo ya kustaafu na wengine walishamaliza likizo, wakajaza fomu maalumu na kupewa hundi za mafao yao, lakini mchakato umesimama.
Msimamo huo wa Serikali, umetajwa kusababisha athari za kiafya kwa waathirika, ambao wengi wamejikuta wakipanga foleni hospitali kupata huduma kutoka na magonjwa na ghafla wanayopata.
Pia taarifa zingine zilieleza kwamba baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakizimia na wengine kupooza kutokana na sintofahamu inayoendelea hivi sasa, kwa sababu hakuna uhakika wa jibu la faraja kwao.
“Kwa kweli watu wanapata matatizo makubwa sana kiafya, katika baadhi ya ofisi tunapata taarifa za wastaafu waliopooza na hii inatokana na kwamba hawajapewa taarifa zenye matumaini,” alieleza mtoa taarifa wetu.
Taarifa zingine kutoka ofisi kadhaa za Serikali, zinaeleza kuwa watumishi wengi wa kada ya chini, ndio waathirika wa uhakiki huo na baadhi wiki iliyopita, walikuwa wakijaribu kukana vyeti walivyokuwa wakitumia.
Taarifa ambazo hazikuthibitishwa kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRL), zilieleza kuwa mafundi wengi wa reli, wamekuwa wakidai kutopata elimu ya sekondari, ili wachukuliwe kuwa wenye ujuzi na elimu ya msingi, lakini kibarua kiendelee.
Wiki iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki alisema utaratibu wa kulipa mafao kwa watumishi hao haujakamilika.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel (CCM), Angela alisema ofisi yake itaandaa utaratibu wa mafao ya wafanyakazi hao.
Awali Amina katika swali lake, alitaka kujua hatua za Serikali zitakazochukuliwa katika kulipa mafao ya wafanyakazi walioachishwa kazi baada ya kukutwa na vyeti bandia.