Leo ni siku ya mama duniani. Kila mzazi anatarajia kupata salamu za shukrani na za upendo kutoka kwa mtoto wake.
Lakini kwa Jenita Japhet, wingu zito la simanzi limeusonga moyo wake baada ya kumpoteza mtoto wake Kelvin Amos (13).
Kelvin, ni miongoni mwa wanafunzi 32 wa Shule ya Msingi Lucky Vicent waliofariki katika ajali ya basi iliyotokea Karatu, Arusha, Mei 6. Wengine waliofariki katika ajali hiyo ni walimu wawili na dereva.
Wanafunzi wengine watatu walijeruhiwa na wanatarajia kwenda Marekani kwa matibabu leo.
Baada ya kupata taarifa za kifo cha mtoto wake, Jenita alizimia kwa saa nane. Alizimia saa tano asubuhi alipopata taarifa za msiba, hadi saa mbili usiku alipozinduka akiwa wodini katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas katikati ya jiji la Arusha.
Kwa mujibu wa wazazi wake, Kelvin alikuwa ni mwanafunzi mwenye juhudi darasani kwani tangu aanze darasa la kwanza amekuwa akishika nafasi tano bora.
Katika mtihani wake wa darasa la saba mwaka huu, alishika nafasi ya tatu kati ya wanafunzi zaidi ya 100.
Mwandishi wetu alifika nyumbani kwake, eneo la Field Force na kumkuta Jenita bado akiwa amegubikwa na simanzi kiasi cha kushindwa kuzungumza vizuri na mumewe, Augustine Amos ndiye aliyekuwa akimsaidia mara kwa mara.
Jenita anakumbuka neno la mwisho aliloambiwa na Kelvin wakati akiingia kwenye basi hilo: “Kwaheri Mama”
Lakini Mungu ameficha siri kubwa katika mauti, Jenita hakujua kuwa kwaheri ile ilikuwa ni ya milele.
Akizungumzia safari iliyochukua uhai wa Kelvin, Jenita alisema mtoto wake alimpa taarifa za safari ya Karatu, Mei 5 saa tatu usiku.
Kelvin aliyekuwa na ndoto ya kuwa daktari, alimweleza kuwa kesho asubuhi (Mei 6) anatarajia kwenda Karatu kwa ajili ya mtihani.
Jenita alisema kutokana na baba yake Kelvin, kuwa Babati kikazi, alimwambia ampigie simu kumpa taarifa lakini Kelvin aliomba yeye (Jenita) ampigie huku akiendelea na maandalizi ya mtihani.
“Nakumbuka alfajiri kama saa 10 hivi, Kelvin aliamka na kuanza kujiandaa mimi, nilishtuka akiwa tayari ameshajiandaa na anataka kuondoka,” alisema.
Alisema alipoamka alimkuta getini anatoka ndipo alipoanza kumfuata nyuma kwani wanaishi jirani na shule.
“Nilimkuta anagonga geti la nyumba nyingine ya jirani, nikamuuliza unafuata nini hapo, akanieleza anampitia mwenzake,” alisema.
Alisema Kelvin akiwa na mwenzake ambaye amesalimika katika ajali hiyo, kwa kuwa alipanda gari jingine, walimwambia arudi nyumbani kwani wapo wawili na watafika shuleni.
“Sikurudi niliamua kuwafuata nyuma hadi shuleni, aliponiona aliniaga ‘kwa heri mama’ na wakapanda kwenye magari mimi nikarudi nyumbani,” alisema.
Alipopata taarifa za ajali, alikwenda shuleni na alipothibitishiwa kuwa Kelvin amefariki alizimia.
“Siwezi kuzungumza zaidi, kazi ya Mungu haina makosa,” alisema.
Baba yake Kelvin
Baba wa Kelvin, Amos ambaye ni mfanyakazi wa Benki ya Posta Babati (TPB Bank PLC), alisema siku ya tukio alikuwa kazini.
Alisema wakati akiendelea na kazi zake, alipigiwa simu na jirani yake saa nne asubuhi akimweleza kuwa gari la shule ya Lucky Vicent limepata ajali.
Hata hivyo, alisema alimweleza jirani huyo, kuwa hadhani kama mtoto wake, ambaye anasoma kutwa alikuwa safarini kwani alikuwa hana taarifa kuwa angekwenda Karatu.
“Ilipofika saa tano hivi, nilianza kuona picha kwenye mitandao watoto wa shule miili yao ikiwa imepangwa kwenye ajali, nilipatwa na hofu nikampigia Mwalimu Onetto,” alisema.
Alisema baada ya kumpigia Mwalimu Onetto alimuulizia Kelvin, kama alikuwa kwenye safari, akaniambia wapo safarini wamepata ajali eneo la Karatu anaweza kuwafuata.
Amos alisema baada ya kupata taarifa hiyo, aliondoka kazini na kuanza safari ya kwenda Karatu.
Alisema akiwa njiani, alipata simu kwa mzazi mwingine mwenye mtoto katika shule hiyo akimwambia kuwa hana sababu ya kwenda eneo la ajali kwani tayari miili imechukuliwa kupelekwa Hospitali ya Mkoa Mount Meru.
“Niliamua kwenda hospitali na baada ya kufika kulikuwa na watu wengi sana hivyo ilikuwa ni vigumu kuingia ndani,” alisema
Hata hivyo, alisema kwa kuwa alikuwa anafahamiana na baadhi ya askari, aliwaeleza yeye ni mzazi na anataka kushuhudia majeruhi na waliofariki kwani kuna mtoto wake.
“Wale askari walinipa ruhusa kuingia ndani na baadaye miili ilifika ambapo nilitambua mwili wa mtoto wangu Kelvin,” alisema
Alisema Kelvin alikuwa ni mtoto wake wa sita na kuna watoto wawili wanaosoma katika shule hiyo; Gladness anayesoma darasa la pili na Glory wa darasa la nne.
Alisema anamkabidhi Mungu yote yaliyotokea kwani kama mtoto wake alipangiwa kufariki katika ajali hiyo hakuna jinsi angeweza kukwepa.
Mwalimu Mkuu azungumza
Alipoulizwa kuhusu ajali hiyo, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Ephraim Jackson alisema taarifa nyingi zinazozungumwa sasa hazina ukweli.
“Nawaomba waandishi muwe makini na taarifa hizi, kwani mambo mengi sana yanaongewa lakini ukweli unajulikana naomba tuyaache hayo,” alisema
Alisema shule hiyo itafunguliwa kesho na akawaomba wazazi kuwapeleka watoto, ili taratibu za masomo ziendelee.
“Huu ni msiba mkubwa ambao umetupata na bado tuna masikitiko makubwa. Ambacho naweza kukuambia sasa ni kuwa shule itafunguliwa Jumatatu,” alisema.
Majeruhi kwenda Marekani
Katika hatua nyingine, wanafunzi watatu ambao walijeruhiwa vibaya katika ajali hiyo wanatarajiwa kupelekwa Marekani kwa ajili ya matibabu leo chini ya ufadhili wa shirika la Stemm la nchi hiyo.
Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alisema jana kuwa tayari hati za kusafiria za wasafiri wote wanane, wakiwamo majeruhi hao watatu, daktari, wazazi wao na muuguzi mmoja zimepatikana.