Ukweli ni kwamba familia nyingi kwa sasa zimekuwa zikiishi na kinadada wa kazi (house girl) ambao ndio kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakishiriki katika kuwatunza watoto nyumbani na kuhakikisha wanakula vizuri na kushinda katika hali ya usalama.
Hivyo ninayofuraha kukumbusha wewe mzazi pamoja na dada wa nyumbani au mlezi mambo haya machache ya kuzingatia katika kuhakikisha usalama wa mtoto wakati wa kula;
1. Jambo la kwanza hakikisha haumuachi mtoto mdogo na chakula au kinywaji bila uangalizi hata kama ni maziwa ya chupa, kama utasahau na kumuacha mtoto katika hali hiyo huweza kusababisha mtoto akapaliwa.
2. Pia usimpe mtoto chakula au maziwa akiwa amelala, analia au anacheka huweza kusababisha mtoto kupaliwa.
3. Epuka kumpa chakula ambacho kinaweza kumkaba au kumpalia hususani karanga, mahindi, zabibu n.k
4. Kabla ya kumpa mtoto chakula hakikisha umekiangalia joto lake usije ukamuunguza mdomo.
5. Mbali na hayo yote, pia usafi wa mtayarishaji, mlishaji na mlishwaji (mtoto) ni muhimu sana katika afya ya mtoto.