MAPYA Yafichuka Ajali Iliyoua Wanafunzi 33 Arusha..!!!


SIRI mpya ya ajali iliyotokea wiki iliyopita na kusababisha vifo vya wanafunzi 33 wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Lucky Vincent, walimu wao wawili na dereva mmoja wa basi, imefichuka baada ya mmiliki wake, Innocent Mushi, kufikishwa mahakamani.

Mushi alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana na kutuhumiwa kutenda makosa manne ya usalama barabarani, yanayodaiwa kusababisha ajali hiyo iliyotokea Mei 6, mwaka huu, baada ya basi walilopanda wanafunzi na walimu wao kutumbukia kwenye korongo lililopo Marera, eneo la Rotia, Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha.

Mushi na mtuhumiwa mwenzake, ambaye ni Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Longino Nkana, walifunguliwa kesi na 78 ya mwaka huu na wanatuhumiwa kwa makosa hayo, likiwamo la kusafirisha watoto bila kuwa na vibali muhimu.

Akiwasomea mashitaka yao mjini hapa mbele ya Hakimu Mkazi Desdery Kamugisha, Wakili wa Serikali, Rose Sule, alidai Mushi, ambaye ni mtuhumiwa wa kwanza, anakabiliwa na makosa manne, wakati Nkana akituhumiwa kwa kosa moja.

Sule alidai kwamba, Mushi akiwa mkurugenzi wa shule hiyo anatuhumiwa kumiliki gari la abiria bila kuwa na leseni ya usafirishaji.

Alidai kuwa Mei 6, mwaka huu, katika eneo la Kwamrombo, wilayani Arusha, mtuhumiwa huyo alifanya shughuli ya usafirishaji wa abiria akiwa anamiliki gari aina ya Mitsubishi Rossa, lenye namba za usajili T871 BYS.

Aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa kosa la pili linalomkabili ni la kuruhusu kuendeshwa kwa gari bila kuwa na bima (road license) ambapo Mei 6, mwaka huu, aliruhusu gari hilo kuendeshwa huku akijua halina bima.

“Kosa la tatu ni kushindwa kuingia mkataba na mwajiri wake, ambapo Mei 6, mwaka huu, ukiwa mmiliki wa gari hilo ulishindwa kuingia mkataba wa ajira na dereva wako, Dismas Gasper, ambaye kwa sasa ni marehemu,” alidai Sule, alipokuwa akisoma mashitaka na kuongeza:

“Mtuhumiwa unakabiliwa na kosa la nne ambalo ni la kubeba abiria waliozidi zaidi ya 13 ambapo Mei 6, mwaka huu ukiwa mkurugenzi, ofisa msafirishaji na mmiliki wa Lucky Vincent, ulibeba na kusafirisha abiria zaidi ya 13, kinyume cha sheria.”

Akisoma mashitaka kwa mtuhumiwa wa pili, Sule alidai mahakamani hapo kuwa, Nkana anadaiwa kuandaa safari iliyozidi abiria 13, huku akijua ni kinyume cha sheria.

Alidai kuwa Mei 6, mwaka huu, mtuhumiwa huyo akiwa na nafasi ya mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo na mwandaaji wa safari aliruhusu kupakia abiria zaidi ya 13 katika gari lililosababisha vifo vya watu.

Kwa upande wake, Wakili Method Kimomogolo, anayewawakilisha watuhumiwa mahakamani hapo, aliiomba mahakama hiyo kuwapa dhamana wateja wake na Sule hakuwa na pingamizi dhidi ya ombi hilo.

Akitoa masharti baada ya kuzisikiliza pande zote mbili, Hakimu Kamugisha alisema washtakiwa hao watatakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaotakiwa kutimiza masharti.

“Mnatakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini dhamana ya shilingi milioni 15. Watuhumiwa mtatakiwa kuwasilisha hati zenu za kusafiria, lakini pia hamtakiwi kuondoka nchini na ndani ya mkoa bila ruhusa ya mahakama,” alisema Kamugisha.

Watuhumiwa wote wawili walifanikiwa kutimiza masharti yaliyotolewa na mahakama hiyo na kesi hiyo sasa itatajwa Juni 8, mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad