Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajia kufanya mazungumzo ya pamoja katika mkutano wa kawaida wa 18 utakaofanyika leo (Jumamosi), Ikulu jijini hapa.
Mkutano huo unatarajiwa kupokea ripoti ya usuluhishi ya kamati inayoongozwa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kuhusu mgogoro wa Burundi.
Mambo mengine yatakayozungumzwa katika mkutano huo ni pamoja na taarifa na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa katika mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo.
Masuala hayo ni pamoja na namna ya kuwezesha uundaji wa magari katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupunguza uagizaji wa magari yaliyotumika kutoka nje ya Jumuiya, mapitio kuhusu sekta ya nguo na ngozi.
Masuala mengine ni pamoja na kuzuia ama kuondoa uagizaji wa nguo na viatu vya mtumba kutoka nje.
Wakuu hao wa Nchi pia wanatarajia kujadili namna endelevu ya uchangiaji wa bajeti ya Jumuiya hiyo kwa nchi wananchama.