Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Zuberi Kabwe amefungukia juu ya Mauaji yanayoendelea mkoani Pwani na kudai maeneo matatu ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji hatajawahi kupatiwa majibu ikiwa ni mtu wa 31 akiwa ameuawa usiku wa kuamkia leo.
Zitto amefunguka hayo baada ya Taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa CCM Tawi la Njia Nne katika Kijiji cha Muyuyu Wilayani Kibiti, Iddy Kirungi, kuthibitishwa kwa mwenyekiti huyo ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
"Eneo la #MKIRU ( Mkuranga, Kibiti, Rufiji) halijapata jawabu la kudumu, Huyu mtu wa 31 kuuwawa eneo Hilo"
Akithibitisha kutokea kwa mauaji hayo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Juma Njwayo,ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji na kusema kwamba, marehemu alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake wakati akijaribu kukimbia.
Bw. Njwayo amesema, kabla ya kuuawa kwa Mwenyekiti huyo, pia wauaji hao walianza kumjeruhi kwa kumpiga risasi ya tumboni mtoto wa marehemu aliyetajwa kwa jina la Nurdin Iddy Kirungi.
Mganga wa zamu katika kituo cha afya Ikwiriri, Dk. Rashid Omar, amesema, walimpokea Nurdin akiwa na jeraha kubwa tumboni mwake ambalo halikutokeza upande wa pili, majeruhi huyo walimpatia rufaa kwenda Hospital ya Mchukwi kutokana na kuwa anavuja damu nyingi sana.