Mshikamano, ndivyo unavyoweza kusema baada ya vichwa vinne kusimama bungeni kuokoa jahazi lisizame kufuatia wabunge kutaka kukwamisha bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Ukiondoa waziri wa wizara hiyo, Charles Mwijage mawaziri waliomuokoa baada ya wabunge kumkomalia kutokana na mianya ya uingiaji wa biadhaa feki nchini kuwachwa bila udhibiti ipasavyo ni Mwigulu Nchemba, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Edwin Ngonyani (Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Seleman Jafo (Naibu Waziri wa Tamisemi) na Luhaga Mpina (Naibu Waziri Muungano na Mazingira).
Hoja ya bidhaa zisizo na ubora iliibuliwa na mbunge wa Wawi (CUF), Ahmed Juma Ngwali na kushika kasi wakati Bunge lilipoketi kama kamati chini ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kupitia vifungu vya bajeti hiyo.
Kutokana na kubanwa huko, Mwijage alitishia kumuomba Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ampe meli aina ya nyambizi ili azizamishe mashua zitakazoingiza bidhaa bandia.
Hata hivyo, majibu ya mawaziri wenzake yalimuokoa maana walishambulia kutoa ufafanuzi uliosababishwa Ngwali aliyekuwa ameshikilia shilingi mpaka ahakikishiwe majibu ya maana, akaamua kukubaliana na hoja zao.