Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe, amejibu swali la Rais John Pombe Magufuli, aliyehoji matumizi ya Sh1.3 bilioni za mfuko wa barabara kwa mwaka wa fedha 2016/2017 katika wilaya hiyo.
Aprili 29 akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Bomang’ombe, Rais alihoji matumizi ya fedha hizo, baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu kumkumbusha ahadi yake ya barabara.
Akiwa katika kampeni za uchaguzi mkuu 2015, Rais Magufuli aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Hai barabara ya lami yenye urefu wa kilometa tano, hivyo Mchomvu akamkumbusha juu ya ahadi hiyo.
Hata hivyo, Rais hakujibu moja kwa moja juu ya ombi hilo, bali alihoji matumizi ya Sh1.3 bilioni za mfuko wa barabara na na kuahidi kumtuma Waziri wa Tamisemi, kuchunguza matumizi yake.
Lakini juzi akiwa katika harambee kuchangia ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Kambi ya Raha, Mbowe alisema kiasi ambacho kimepokelewa na halmashauri ni Sh300 milioni na siyo Sh1.3 bilioni.
“Wakati wa ziara Rais aliuliza kiasi ambacho tumekwishapatiwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara lakini kwa bahati mbaya waliompatia taarifa wakampatia taarifa isiyo sahihi,”alisema Mbowe.