Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba amefunguka na kusema jambo alilofanya Rais Magufuli kuzuia mchanga litakwenda kuigwa duniani kote na kuleta mapinduzi katika "Extractive Industries" (sekta za uchimbaji madini)
Serukamba alisema hayo jana bungeni na kusema ukiona mpinzani wako anakupinga katika jambo lolote lile basi ujue umefanya jambo ambalo ni sahihi ila ukiona mpinzani wako anakusifu ujue umefanya jambo baya, hivyo kwa kuwa wapinzani wanalalamika basi Rais amepatia katika maamuzi yake, na anatakiwa kupewa ushirikiano wa wananchi na wabunge.
"Mimi kama mwanasiasa ukiona mtu ambaye ni adui yako umefanya jambo akakusifia ujue lipo tatizo, ila ukiona umefanya jambo adui yako akasema umekosea maana yake umepatia sana. Mimi naomba nimpongeze Rais Magufuli kwa kazi kubwa aliyofanya na niwaambie waheshimiwa wabunge, duniani kote 'Extractive Industries' inaenda kubadilika atakaye kuwa kwenye historia ya kubadilisha Extractive Industries ni Rais Magufuli, leo duniani kote kila kwenye migodi mambo yatabadilika kwa sababu ya Magufuli amefungua milango, niwaambieni watanzania tusiogope kwenye hili lazima tuwe nyuma ya Rais tumuunge mkono aendelee na nina hakika wawekezaji watakuja mezani" alisisitiza Serukamba