MBUNGE wa Viti Maalum (Chadema), Catherine Ruge, jana aliuliza swali muda mfupi baada ya kuapishwa, akifuata nyayo za Salma Kikwete, mke wa Rais mstaafu ambaye ni Mbunge wa kuteuliwa.
Baada ya kuapishwa katika siku ya kwanza ya Bunge hili la bajeti Aprili 5, mke wa Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, Salma hakupoteza muda kutaka kujua mpango mahususi wa serikali wa kuongeza usambazaji wa huduma ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini(TASAF) kwa watu maskini mkoani Lindi.
Si kawaida kwa wabunge wanaoapishwa siku hiyo kuuliza maswali, lakini muda mfupi baadaye jana, Ruge alihoji mkakati wa serikali wa kukuza utalii kwa upande wa magharibi wa mbuga ya Serengeti iliyopo mkoani Mara; ambao umeonekana kusahaulika.
Ruge aliuliza swali hilo la nyongeza kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, muda mfupi baada ya kuapishwa na Spika Job Ndugai.
Mbunge huyo alisema upande huo unaonekana umesahaulika, lakini una vivutio vingi vya utalii na hasa Ziwa Victoria, lakini pia kuna visiwa.
“Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa iliyobarikiwa kuwa na vivutio vya utalii vikubwa ikiwamo mbuga ya Serengeti kwa upande wa mashariki,” alisema Ruge.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ramo Makani, alisema eneo linalopakana na Serengeti kwa upande wa magharibi ni kati ya maeneo ambayo serikali imeshaweka mipango thabiti ya kuboresha.
“Serengeti ipo milango ya kuingia ambayo mingi inatokea mkoa wa Arusha, lakini tumeshaangalia hili sasa kutakuwapo ya kutokea mkoa wa Mara, na Shinyanga tutaboresha mageti ili watalii waingie kwenye kona zote ili kuruhusu idadi kubwa ya watalii kuingia,” alisema Makani.
Alisema serikali ipo mbioni kuboresha maeneo hayo na kumkaribisha wizarani kutoa maoni ya kuboresha eneo hilo.
Ruge aliapishwa jana kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Dk. Elly Macha, ambaye alifariki dunia nchini Uingereza mwezi mmoja uliopita.