MEYA wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro na pia baadhi ya madiwani na viongozi wa dini waliokamatwa katika tukio la kutoa misaada kwenye shule ya Lucky Vincent iliyopo mjini Arusha sasa wako katika hatari ya kufikishwa mahakamani kukabiliana na mashtaka.
Hata hivyo, hatua hiyo ya kushtakiwa kwa viongozi hao itatokana na matokeo ya uchunguzi unaoendelea kufanywa na jeshi la polisi na hivyo, bado haijawekwa wazi ni makosa gani watakabiliana nayo pindi wakifikishwa kortini.
Viongozi hao na ujumbe wao wenye jumla ya watu 13 walikamatwa juzi wakati wakiwa katika Shule ya Awali na Msingi ya Lucky Vincent na hadi kufikia jana jioni, bado walikuwa wakishikiliwa katika mahabusu ya polisi.
Wengine wanaotajwa kuwamo katika kundi hilo ni pamoja na viongozi wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco), Kanda ya Kaskazini. Walikwenda shuleni hapo kutoa rambirambi kutokana na tukio lililohuzunisha taifa hivi karibuni la ajali ya basi la shule hiyo, iliyopoteza maisha ya watu 35, wakiwamo wanafunzi 32.
Aliyeashiria kuwapo kwa uwezekano wa kushtakiwa kwa viongozi hao ni Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembu, aliyeiambia Nipashe jana kuwa bado wanawashikilia watu 13 waliowakamata juzi.
Kamanda Ilembu aliongeza kuwa hadi kufikia jana, bado walikuwa wakiendelea kuwahoji masuala kadhaa wahusika ili baadaye taratibu zingine zifuate, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani au vinginevyo.
Aidha, Kamanda Ilembu alikataa kuwataja majina watuhumiwa wanaowashikilia kwa maelezo kuwa bado wanaendelea kuwahoji.
Hata hivyo, waliokuwapo katika tukio la kutoa rambirambi juzi kwenye shule hiyo ya Lucky Vincent walifahamika kuwa ni pamoja na Meya Lazaro na viongozi kadhaa wa dini.
Rambirambi iliyotarajiwa kutolewa ilifuatia ajali hiyo ya gari ya Mei 6, mwaka huu na kuwaua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva waliokuwa wakienda kufanya mitihani ya ujirani mwema na wanafunzi wenzao wa darasa la saba wa Shule ya Tumaini Junior iliyoko wilayani Karatu.
Hata hivyo, rambirambi hiyo haikuweza kutolewa baada ya polisi kuwakamata kwa kile kilichoelezwa na Kamanda Ilembu kuwa wahusika walifanya mkusanyiko/mkutano usio na kibali katika eneo hilo.
Pia katika tukio hilo, waandishi wa habari 10 walikamatwa pia na kuachiwa muda mfupi baada ya kufikishwa kituo kikuu cha polisi cha mkoa.