ALIYEKUWA Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai, ambaye anadaiwa kukutwa na mali za thamani zaidi ya Sh. bilioni 3.5 sasa anaweza kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Chanzo cha uhakika kimeiambia Nipashe kuwa mojawapo ya kosa litakalompeleka mahakamani kigogo huyo wa zamani wa Takukuru, ni kosa la kujilimbikizia mali kinyume cha maadili ya utumishi wa umma. Pia mali hizo zinahusishwa na tuhuma za rushwa.
Kwa mujibu wa tangazo la Takukuru jana, mali za mhasibu huyo wa zamani ni pamoja na nyumba saba za maghorofa zilizopo katika maeneo ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam; nyumba tisa za kawaida zikiwamo zilizopo kwenye maeneo mbalimbali ya majiji ya Dar es Salaam na Mwanza na pia Musoma mkoani Mara; viwanja 37 vikiwamo vya kwenye maeneo ya karibu mwa bahari ya Bagamoyo, Ununio, Mbweni na Kigamboni; magari matano na pikipiki moja ambavyo kwa pamoja, thamani yake inakadiriwa kuwa zaidi ya Sh. bilioni 3.5.
Chanzo hicho ndani ya Takukuru kiliiambia Nipashe jana kuwa taratibu zinakamilishwa na mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yake wakati wowote kuanzia sasa.
“Yuko mbioni kushtakiwa. Na ndiyo maana lile tangazo limetolewa kwenye magazeti… ukiona tangazo kama lile ujue huyo mtu karibu anashtakiwa,” alisema mtoa taarifa huyo kwa sharti la kutotajwa jina.
“Siwezi kusema ni lini hasa atafikishwa mahakamani. Lakini naweza kukuthibitishia kuwa siku si nyingi… ni suala la kusubiri tu,” chanzo kilisema na kuongeza:
“Mahakama haiwezi kutoa oda ya kuzua mali ya mtu kama hujaishawishi. Lazima uishawishi mahakama kwamba mtu unayemtuhumu yuko mbioni kushtakiwa na ndipo wanakupa oda ya kuzuia mali zake. Kwa hiyo hilo ndilo lililopo kwa sasa. ”
Mei 9 mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilitoa amri ya zuio la mali za Gugai ambaye anakabiliwa na tuhuma za limbikizo la mali kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Namba 11 ya mwaka 2007.
Amri ya zuio la mali za Gugai imetolewa na mahakama hiyo kufuatia ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) chini ya kifungu namba 38(1)(a) na (b) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007 katika shauri namba 13 la 2017.
Kufuatia maombi ya DPP, mahakama imeamuru mali zilizotajwa kuwa za Gugai ziwe chini ya zuio la mahakama.
Pia mawakala wake na watu wengine wote wanaomwakilisha wamezuiwa kuuza au kuhamisha umiliki au kuweka dhamana mali zote zilizowekewa zuio.
Aidha, msajili wa hati ameagizwa kusajili zuio hilo kama kizuizi dhidi ya mali zote zilizotajwa.
Pia Msajili Msaidizi wa magari ameagizwa asiruhusu uhamishaji wa umiliki wa vyombo vya moto vilivyowekewa zuio mpaka mahakama itakapoelekeza.
MALI ZENYEWE
Orodha ya mali zilizowekewa zuio la mahakama ni pamoja na nyumba nne za ghorofa moja zilizoko kiwanja na 64 Kitalu B, Ununio, Kinondoni; nyumba tatu za ghorofa moja zilizoko kiwanja na 150 Kitalu 8 Bunju, Kinondoni na nyumba nne zilizoko kiwanja namba 225 kitalu 6, Mbweni JKT, Kinondoni.
Nyingine ni nyumba zilizoko kwenye kiwanja namba 62 na 63 kitalu C, Kinondoni; nyumba iliyoko kiwanja namba 29 kitalu L, Majita, Musoma mkoani Mara; nyumba namba 713 PPF Kiseke, Mwanza na nyumba iliyoko kwenye kiwaja namba 438 kitalu D, Nyegezi, Mwanza.
Aidha, viwanja ni pamoja na kiwanja namba 14 kitalu J, Bunju, Kinondoni; kiwanja namba 47 kitalu B, Mwongozo, Kigamboni; kiwanja namba 184 kitalu B, Buyuni,Temeke; kiwanja namba 103 kitalu L, Kaole, Bagamoyo; kiwanja namba 104 kitalu L, Kaole, Bagamoyo na kiwanja namba 209 kitalu B, Kibaha.
Vingine ni kiwanja namba 195 kitalu 3, Kihonda, Morogoro; kiwanja namba 993 kitalu L, Kiegeya, Morogoro; kiwanja namba 868 kitalu Q, Lukobe, Morogoro; kiwanja namba 34 kitalu K, Kisasa B, Dodoma; kiwanja namba 32 kitalu N, Itega, Dodoma; kiwanja namba 39 kitalu M, Itega, Dodoma; kiwanja namba 24 kitalu B, Chidachi, Dodoma; kiwanja namba 64 Nzuguni, Dodoma; kiwanja namba 230 kitalu B, Nyegezi, Mwanza na kiwanja namba 439 kitalu D, Nyegezi, Mwanza.
Viwanja vingine ni kiwanja namba 275 Kitalu 2, Nyamhongolo, Mwanza; kiwanja namba 277 kitalu 2 Nyamhongolo, Mwanza; kiwanja namba 296 kitalu 2, Nyamhongolo, Mwanza; kiwanja namba 297 kitalu 2, Nyamhongolo, Mwanza; kiwanja namba 286 kitalu G, Nyamagana, Mwanza, kiwanja namba 287 kitalu G, Nyamagana, Mwanza; kiwanja namba 90 kitalu 5, Bugarika, Mwanza; kiwanja namba 126 kitalu A, Makoko, Musoma; kiwanja namba 622 kitalu A, Gomba, Arusha; kiwanja namba 621 na 623, kitalu A, Gomba, Arusha; kiwanja namba 737 kitalu C, Mwambani, Tanga; Kiwanja namba 1,2 na 3 kitalu J,
Mwambani,Tanga; kiwanja namba 4 kitalu J Mwambani, Tanga; kiwanja namba 5 kitalu J, Mwambani Tanga; kiwanja namba 18 kitalu J, Mwambani, Tanga; kiwanja namba 79 kitalu J, Mwakidila, Tanga; na kiwanja namba 11 13 kitalu J, Mwakidila, Tanga.
Magari yaliyozuiwa ni matano, ambayo ni gari namba T 180 DBQ, Mitsubish Canter; gari namba T 581 BQU, Toyota Hillux; gari namba T 814 CSC , Nissan Murrano; gari namba T 679 ASD Toyota RAV 4; gari namba T 913 DHE Suzuki na pikipiki namba MC 837BCL.
Credit - Nipashe