BUNGE limeishauri serikali kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) baada ya kubaini wanafunzi wengi watakosa fedha hizo mwakani kutokana na bajeti ndogo iliyotengwa.
Ushauri huo ulitolewa bungeni mjini hapa juzi na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipokuwa ikiwasilisha taarifa yake kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.
Akiwasilisha taarifa hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, Hussein Bashe, alisema wamebaini wanafunzi wengi watakosa mikopo mwaka ujao wa fedha licha ya kuwa na ufaulu mzuri.
Alisema mwaka huu wa fedha wanafunzi 48,502 walijaza fomu kwa ukamilifu lakini 25,555 tu ndiyo walipata mikopo na hivyo kuacha wengine 22,947 wakiwa hawana mikopo kutokana na bajeti iliyotengwa ya Sh. bilioni 427.5 kutotosheleza mahitaji.
Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), alisema mwaka ujao wa fedha HESLB imeombewa Sh. bilioni 427.5 (sawa na bajeti ya mwaka huu) ilhali ufaulu wa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita umeongezeka kutoka asilimia 88 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 99 mwaka huu.
"Kamati inaona kwamba, suala la elimu ya juu ni haki ya msingi kwa watu wenye sifa," alisema.
"Kamati inashauri serikali kuongeza bajeti ya HESLB ili wanafunzi wengi zaidi wanaostahili waweze kupata mikopo kwa maendeleo ya taifa letu."