Wakili Alberto Msando amejiuzulu nafasi yake ya ushauri wa Chama cha ACT-Wazalendo.
Taarifa iliyotolewa jana, Jumanne na kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe imeeleza kuwa Msando ameandika barua ya kujivua wadhfa huo ambayo imepokelewa na chama hicho.
“Ndugu Msando anawajibika kwani anapaswa, nanukuu ‘kuishi Kama mfano Kwa jamii inayonizunguka.’Chama kinamshukuru kwa moyo wake wa kuzalendo na mchango alioutoa katika Chama. Ni matumaini yetu ataendelea kushirikiana nasi katika ujenzi wa chama kwa kadri atakavyoweza na atakapohitajika kama mwanachama,”amesema Zitto.
Zitto amesema Msando amekuwa kiongozi mwenye mchango mkubwa katika chama katika nafasi mbalimbali alizoshika ndani ya ACT.
“Nikiwa Kiongozi wa Chama nimekubali kuwajibika kwake na kumtakia kheri katika kujisahihisha kwake. Msando ameomba msamaha kwa jamii kwa uwazi na ni wajibu wetu kumsaidia kupita katika mitihani iliyomkumba,”amesema Zitto.