Mbunge wa Geita Vijijini(CCM), Joseph Kasheku 'Msukuma' amesema ni wabunge wawili au watatu ambao tu ndiyo ambao hawakupita kwa waganga wa kienyeji wakati wa uchaguzi.
Msukuma aliyekuwa anauliza swali la nyongeza bungeni, amesema wabunge wamekuwa na tabia ya kuwatetea wasanii waliowasaidia kwenye uchaguzi, lakini ukifika kwa waganga wa kienyeji wanakaa kimya wanapopata matatizo.
Msukuma ambaye Naibu Spika amemtaja kama mwakilishi wa waganga wa jadi, ameuliza kwa nini kisianzishwe chuo cha kuwapatia waganga hao mafunzo.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema waganga hao ni muhimu kwa kuwa asilimia 60 ya Watanzania wanatumia tiba zao mbadala.
Amesema wizara inaendelea kutoa elimu na imewaagiza waganga wakuu wa wilaya kuwa wasajili wa waganga wa jadi.