Vifo hivyo vyote vimetokana na maporomoko ya maji, mawe, miti na mchanga kutoka katika Milima ya Usambara Magharibi ambavyo vimeendelea kuvamia kwa kasi baadhi ya nyumba zilizo mabondeni katika kata za Mkumbara, Chekereni, Makuyuni, Kwagunda, Kerenge na Ngombezi.
Pia Imebainika kwamba hali ya usalama kwa baadhi ya wananchi imekuwa tete hasa wale wanaokaidi agizo la serikali linalowataka kuhama badala yake wanaendelea kung’ang’ania kuishi ndani ya nyumba zao zilizoko bondeni jirani na kingo za Mto Pangani kwa kuwa tayari wanyama wakali akiwemo mamba wameanza kutumia mafuriko hayo kuvamia nyumba hizo ili kutafuta malisho.
Akizungumza jana jioni katika mahojiano kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel alisema hali ya uslama kwa wakazi wa maeneo hayo haijatengemaa hivyo jamii inapaswa kufanya kila linalowezekana ili kuokoa maisha.
“Kuna tukio la kusikitisha sana la jana huko Kata ya Ngombezi ambako ni jirani na mto Pangani kuna mama mmoja amenusurika kuliwa na Mamba wakati alipokuwa akisafisha kifaa cha kudekia nyumba kwa kutumia maji hayo ya mafuriko,” alisema mkuu wa wilaya na kuongeza: “Ilikuwa tu baada ya kumaliza usafi akaamua kwenda kusuuza dekio bila kujua kwamba kumbe mamba alikuwa mawindoni ametoka huko mtoni na kujichanganya kwenye hayo mafuriko jirani na nyumba wakati mama akiendelea kusafisha ndipo mamba akavamia hilo dekio na kuondoka nalo na mama akanusurika.
Hii ni hatari nawahimiza watii agizo la serikali ili tuokoe maisha kwa kukubali kuhamia maeneo makavu ya juu milimani.” Alisema kitendo cha mama kuvamiwa na mamba kutokana na mafuriko kuendelea kuzingira nyumba ni kiashiria tosha kwamba maji yanapoingia ndani na mamba nao wanahamia katika makazi ya wananchi hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kuchukua tahadhari.
Aidha, alitaja athari nyingine zilizopatikana ni kufungwa mara kwa mara kwa baadhi ya barabara kuu na kusababisha baadhi ya magari na watumiaji wengine kusubiri kwa muda wakati maporomoko ya maji na mawe yanapokatiza kwenye maeneo hayo.
Alisema mpaka sasa tathmini halisi ya hasara iliyosababishwa na maafa hayo bado haijapatikana kwa kuwa kamati ya wilaya inatarajia kukutana kesho. Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani Tanga, Alfred Ndumbaro akizungumzia madhara yaliyotokea katika baadhi ya barabara kuu kutokana na mafuriko hayo, alisema wao wamefanikiwa kuondoa vikwazo barabarani ili gari ziendelee kupitika.
“Kikosi kazi chetu kinashughulikia maeneo ya Mazinde na Mkumbara katika barabara kuu ya Segera - Mkumbara ili kuhakikisha miundombinu hiyo inarejea katika matumizi yake ya kawaida,” alieleza Ndumbaro baada ya magari kukwama kwa muda eneo la Mazinde.
Hata hivyo, alitaja maeneo mengine ambayo yanaendelea kushughulikiwa ni katika barabara kuu ya Mombo - Lushoto ambako vifusi vya udongo vilianguka kutoka juu milimani na kuziba njia katika baadhi maeneo.
Kuhusu barabara kuu ya Tanga – Pangani, alisema Tanroads inafanya juhudi za haraka za kuchepusha barabara katika maeneo yaliyoharibika ikiwemo karibu na daraja la Neema ili kuwezesha watumiaji kuendelea kupata huduma wakati serikali ikiangalia njia ya muda mrefu ya kutengeneza eneo hilo.
Mmoja wa wasafiri waliokuwa wakitoka Moshi, Jacob Tesha alieleza kuwa walikwama Mazinde tangu saa tano asubuhi, na walipewa taarifa na Polisi wa Mazinde kuwa Mombo barabara imeharibika na magari yamezuiliwa na wao walizuiliwa Mazinde. Alisema foleni ilikuwa ya mamia ya magari.
Alisema njia ilianza kufunguliwa saa 11 jioni, na akaeleza kuwa makalavati ya eneo la Mombo ni madogo, hivyo maji yamefurika na kuharibu njia. Wakati huo huo watu watano wamejeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Lushoto baada ya magari matano waliyokuwa wakisafiria kati ya miji ya Soni na Lushoto mkoani Tanga kuangukiwa na kifusi cha udongo na mawe.
Magari hayo ambayo namba zake za usajili hazikuweza kupatikana mara moja ni mabasi mawili aina ya Costa, Toyota Carina moja, Noah moja pamoja na Hilux moja ambayo inamilikiwa na shirika La umeme Tanesco wilayani Lushoto.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amethibitisha tukio na kuongeza usiku huu jana askari wa jeshi la Polisi wilayani Korogwe wamelazimika kufunga baadhi ya maeneo ya barabara kuu ikiwemo ya Mombo - Mkumbara - Mazinde wilayani Korogwe ili kuepusha madhara kutokana na ongezeko la maporomoko ya maji, tope, na miti kufuatia mvua nyingi zinazoendelea kunyesha.