Mwalimu Atiwa Mbaroni Baada ya Kuiba Mtoto Mchanga Hospitalini
0
May 13, 2017
JESHI la Polisi mkoani Songwe linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Msingi Majengo, mkazi wa Songa katika Halmashauri ya mji wa Tunduma, (jina linahifadhiwa) kwa tuhuma za kuiba mtoto mchanga wa siku moja.
Mtoto huyo aliibwa katika wodi ya wazazi kwenye Hospitali ya Wilaya Mbozi mjini Vwawa.
Roida Salimu, ambaye ni shuhuda wa tukio hilo, alisema mwanamke huyo aliingia wodi hiyo kwa njia ya kificho muda usiojulikana akiwa amejifunga nguo tumboni kama mjamzito anayetarajia kujifungua na pia hakuwa na kadi ya kliniki.
Alisema baada ya kumwiba mtoto huyo alimficha chooni nyuma ya mlango akiwa amemviringisha nguo wakati akitafuta njia
ya kutokomea naye.
Alisema mama mzazi wa mtoto huyo ambaye alijifungua watoto mapacha wote wakiume, alishtuka kuwa mtoto mmoja hayupo kitandani muda wa saa
10:00 alfariji Mei 11 mwaka huu na kutoa taarifa kwa muuguzi wa zamu ndipo jitihada za kumtafuta zilianza.
Mganga Mkuu Wilaya ya Mbozi, Janeth Makoye, alikiri kukamatwa kwa mama huyo katika hospitari hiyo na kuwa mama mwenye mtoto ni mama wa
miaka 17, mkazi wa Kamsamba wilayani Momba .
Alisema baada ya kujifungua Mei 10 mwaka huu, alikuwa akisubiri kuruhusiwa na watoto wake mapacha wote wakiwa wakiume wakiwa na umri wa siku moja.
Alisema ni utaratibu mama mjamzito akijifungua lazima awe kwenye uangalizi wa saa 24 ili kufuatilia afya ya mama na mtoto kama wako salama kabla ya kuwaruhusu.
Aidha, alisema kuwa elimu kwa jamii inatakiwa kutolewa hasa kwa wale wasio kuwa na uwezo wa kuzaa ama kutungisha mimba ili kufika katika
vituo vya afya na kupima kwani wanawake wamekuwa wakinyanyaswa bila kujua kati ya mama au baba nani ana tatizo.
Atupele Gabriel, alisema tukio hilo liwe fundisho na hatua madhubuti za kuimarisha ulinzi hospitalini hapo zichukuliwe kwa kujenga uzio wa
ukuta badala ya uzio wa senyenge uliopo ambao unatoa nafasi mharifu kupenya.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi, mkoani hapa Ambwene Mwanyasi, alisema kuwa mwanamke huyo alikamatwa Mei
11 mwaka huu saa 11 alfajiri akijaribu kutoroka na mtoto huyo wa jinsia ya kiume.
Mwanyasi aliongeza kuwa mama huyo alijifunga nguo tumboni ili aonekane ana ujauzito na kwenda wodini bila kupitia mapokezi.
Kamanda alisema mahojiano yalionyesha kuwa chanzo cha tukio hilo mwanamke huyo kunyanyaswa na mume wake kwa kutozaa ndipo alipoamua kufanya tukio hilo ili kunusuru ndoa yake.
Tags