Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba amesisitiza kuwa changamoto ya mauji ya watu mkoani Pwani iko mbioni kutatuliwa kwa kuwa serikali imeshabaini wanaofanya mauaji hayo ni watu wanaotoka kwenye maeneo ya Kitibi, Mkuranga na Rufiji.
Mwigulu aliyasema hayo leo Bungeni mjini Dodoma wakati akitoa maelezo juu ya matukio yanayoendelea mkoa wa Pwani.
Alisema kuwa kamata kamata itaendelea katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji hadi wahalifu wote watakapokamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.
Awali Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini aliomba Bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili hali ya amani katika maeneo hayo.
"Kwa sasa watu wanakamatwa hovyo na polisi katika maeneo hayo na mfano kijana Sultan Mpigi aliyekamatwa na polisi akiwa mzima lakini maiti yake ilikutwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili". Alisema Selasini.