My Story: Nilivyojikuta Naupenda Ukimwi Alioupata Mpenzi Wangu na Kilio Chake..Sehemu ya Kwanza..!!!!


Na Edward Lucas

Utamu wa tendo la ndoa umepewa upekee wa kutolinganishwa na chakula chochote duniani, lakini kumbukumbu ya tendo hilo hutofautiana sana kati ya mwanaume na mwanamke. Utanielewa ukiendelea…

Binafsi nakumbuka sana utani wa rafiki yangu tuliyemtania kwa jina la ‘Ngoswe’, ambaye aliwahi kutuambia, “Unajua ni rahisi sana mwanamke hata aliyezeeka kukumbuka alijisikiaje mara ya kwanza kufanya mapenzi akiwa na miaka 20 hivi. Lakini ni vigumu sana kwa mwanaume aliyefanya mapenzi mara kadhaa, kukumbuka vizuri utofauti aliousikia alipofanya tendo hilo kwa mara ya kwanza.”

Ngoswe alitumia maneno yenye ukakasi kunilazimisha kuelewa alichokuwa anazungumzia ili nifahamu kuhusu mahusiano ya mapenzi aliponiona nimezama katikati ya kina cha penzi la mrembo mmoja aliyeniendesha kama gari lililokata break kwenye mteremko.

Huyo jamaa alinambia kuwa kinachoshangaza, katika maisha ya uhusiano, utamfanyia mwanamke kila kitu unachotaka, lakini kumbuka kuwa kwa kiasi kikubwa kumbukumbu yake hufutika na kurejea upya kana kwamba mmeanza jana tu. Sikumuelewa hadi yaliponikuta na kujikuta nikishindwa kusikitika hata kidogo nilipoambiwa kuwa mpenzi wangu ameambukizwa virusi vya ukimwi.

Najua wengi watashtuka sana kwa neno hili hasa wakijiuliza inakuaje mtu afurahi wakati mwenzie yuko kwenye matatizo. Lakini kwa upande wangu ni ngumu sana kudanganya kwa nafsi yangu kuitangaza huzuni isiyokuwa moyoni mwangu.

Nakumbuka siku ile aliyonitamkia kwamba hanihitaji tena alisema hakuna marefu yasiyo na ncha na kwamba amekaa na kutafakari kwa kina na kuona mimi siendani naye na kwa maana hiyo nitafute msichana mwingine na kama siwezi basi niwe ‘padre’. Daaaah!!!! iliniuma sana.

Nilisoma ujumbe wake wa kunikataa nikiwa kazini, nafundisha wanafunzi darasani huku kiu kali ya maji ikiniunguza koo kutokana na uhaba wa maji katika kijiji nilichopangiwa. Na sio tu kwamba kulikuwa na uhaba wa maji, mimi pekee ndiye mwalimu niliyekuwa nachagua sana maji ya kunywa, ‘lazima yawe yamechemshwa’ hivyo kuyapata pia ilikuwa mtihani zaidi.

Nilipomaliza kuusoma ujumbe wake, kwakweli nilishindwa kuuhisi ulimi mdomoni kwangu…mate yalinikauka ghafla. Ilibidi kipindi kiishie palepale..!

‘Nimeamua kuishi peke yangu, I need to be alone. Naomba uniache, tafuta mwanamke mwingine, mwalimu mwenzako atakuwa hadhi yako nadhani..! Ukishindwa unaweza kuwa padre mzuri,” ilisomeka sehemu ya ujumbe wake.

Haya yanaweza kuonekana ni maneno ya kawaida sana…lakini yalitoka kwa mtu niliyeweza kuwa naye katika mahusiano kwa zaidi ya miaka sita (6) na nikatumia nguvu kubwa ya kiuchumi kumsaidia katika elimu yake ya Chuo Kikuu. Baada ya kuhitimu, hii ndo zawadi ya maneno aliyoniandalia kwa muda wote huo. Kumbe tulikuwa wawili, mimi nikacheza nikijua ndio kila kitu.

Mwanzoni nilidhani anatania. Lakini kwa jinsi alivyosisitiza nikaanza kujiuliza kuna jambo gani baya lililomtatiza juu yangu hadi amepata maneno makali hivyo!! Akili nyingine ilinituma labda kuna mtu kamjaza habari za uongo juu yangu…lakini katika tafakari na kudadisi nilikuta hakuna kitu kama hicho.

Hii ilikuwa ni miezi miwili tu tangu ahitimu masomo yake ya Chuo Kikuu na kwa mipangilio na makubaliano yetu ni kwamba baada ya kuhitimu tutafanya taratibu za kuishi pamoja katika ndoa. Sikujua nilikuwa naota ndoto,  alinacha kwenye dunia ya Abunuasi.

Hili jambo liliniuma sana na kuanza kujiuliza kipi kipya sana kimeongezeka kwake hadi kuhisi siendani naye!!! Ni kwanini kwa kipindi chote hicho asiniambie kwamba hatuendani ili nitafute huyo wa ‘saizi’ yangu? Hadi amesubiri…nimehudumia kwa jasho kubwa na kazi yangu mshahara kiduchu, amehitimu chuo ndio anasema hivi. It’s so painful!

Haya mambo niliwahi kuyasikia kwenye wimbo mmoja wa zamani sana. Nikajua ni utunzi tu. Mwisho yakanikuta mwenyewe.

Siku tatu baadae, ambayo pia ni siku ya tatu baada ya kumaliza mitihani yake alinambia hataki tena simu kutoka kwangu wala meseji na kama nitakuwa na ujumbe basi nimpatie rafiki yake aliyekuwa akiishi naye hosteli atamfikishia…nilipomuuliza sababu za maamuzi hayo alinijibu kwa ufupi, “ukija tutaongea”. Na siku aliyokuja baada ya hiyo miezi miwili aliyokuja nayo ndio hayo.

Siku ya tatu iliwadia, nilijipanga sana kumshawishi ausikie moyo wangu. Lakini alisisitiza tena kwamba hahitaji nimpigie simu wala kumtumia meseji kwa sababu hayuko tayari kuwa katika mahusiano na mtu yeyote…na kweli zilipita siku mbili nikiwa bize kumtafuta katika simu bila majibu.

Nilipoendelea sana, niligeuka kuwa usumbufu kwake.

Itaendelea Kesho....!!!

Utunzi wa Edward Lucas; 0655 545 064

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad