My Story: Nilivyojikuta Naupenda Ukimwi Alioupata Mpenzi Wangu na Kilio Chake (Sehemu ya Pili 2)..!!!


Inaendelea....!!!

Siku ya tatu iliwadia, nilijipanga sana kumshawishi ausikie moyo wangu. Lakini alisisitiza tena kwamba hahitaji nimpigie simu wala kumtumia meseji kwa sababu hayuko tayari kuwa katika mahusiano na mtu yeyote…na kweli zilipita siku mbili nikiwa bize kumtafuta katika simu bila majibu.

Nilipoendelea sana, niligeuka kuwa usumbufu kwake.

“We mwanaume… kwanini tunasumbuana hivi?? Unanimalizia chaji, nikwambie kwa lugha gani? Hivi huna kazi za kufanya au ndugu wa kuwapigia simu?” alinambia kwa ukali sana.

“Naomba nikwambie ukweli tu ndugu yangu…mimi nina mtu mwingine ambaye amekwisha nitolea mahari, sasa tayari unajua kinachofuata, tusiharibiane please.”

Kufikia hapo moyo ulishituka mithili ya sahani nzuri za udongo zilizodondoka kwenye vigae imara. Nilitaka kupiga kelele kwa sauti kama aliyeona jinamizi, Duuu!!! Kweli nilikubali kutoka jasho na kuhema sana sio lazima uwe umekimbia au kubeba mzigo.

Kipindi nikiwa bado nimepigwa ganzi ya maneno hayo.. nilimsikia akiendelea kuongea na kusema “tafadhali!! usipige simu yangu ovyo utaniharibia ndoa yangu……mimi sasa nina mume tena mpole kama huamini basi muulize mtu yeyote wa karibu yangu atakwambia…so jiheshimu” kisha akakata simu.

Hadi kufikia hapo kwa wale waliowahi kukutana na hali hiyo naamini wanayatambua maumivu hayo…kwahiyo wanaweza kuyahisi maumivu niliyokuwa nayo kwa wakati huo. Kiufupi tu ni kwamba inauma zaidi ya sana.

Machozi yalianza kunitiririka. Nilikunja sura na kulia kama mtoto aliyefinywa. Nikijiuliza, muda wote nimepigwa na vumbi la chaki, nimeamka asubuhi na mapema, nimejinyima kwa kila namna ili niweze kutimiza ndoto za mpenzi wangu katika elimu yake lakini hatua ya mwisho ananiambia tayari yeye ni mchumba wa mtu na tayari mahari kishatolewa!! Kwahiyo nilimsomeshea mwanaume mwingine!

Nilijiuliza kama amepata mchumba hata wa kufikia kumtolea mahari basi mahusiano yao yalianza kitambo kidogo. Sasa kwanini muda wote alikuwa akiomba pesa kutoka kwangu?? Hata hatua ya mwisho aliomba nauli kutoka kwangu akamalizie mitihani yake, kwanini asingemuomba huyo mchumba wake?

Basi… zilipita kama siku tatu pasipo kumtafuta huku nikiwa katika wimbi kubwa la mawazo hatimaye nilishindwa kujiuzuia na kuamua kumpigia simu….lakini maneno yaliyotoka hapo hadi nilijuta kupiga simu.

Baada ya simu kuita mara kadhaa bila majibu hatimaye alipokea na kusema kwa lugha ya ukali sana “hivi wewe!! unataka kunambia hata mama yako alishafariki umeshindwa kumpigia simu umekaa kunisumbua mimi? aliweka pozi kidogo kisha akaendelea

“Hivi vyalimu navyo sijui vipi……havielewi! Sijui huko darasani vinafundisha nini, We si nimekwambia sitaki unipigie simu wala kunitumia meseji au hadi nibadili hii namba kwa ajili yako ndio ujue namaanisha ninachokisema!? Alimaliza kwa kunisonya kisha akakata simu.

Daaaa!!!! kufikia hapo nilijihisi kama vile pakiti ya chumvi imesiginwa kwenye kidonda kibichi tena bila huruma.

Nikijiuliza huo ualimu wangu ulivyofanya kazi kubwa kumlipia ada na mahitaji mengine ya shule na awapo nyumbani..leo hii ualimu kwake ni kama tusi na ni kazi ya kudharaulika, kweli waswahili walisema bora umfadhili mbuzi unaweza kuambulia hata mchuzi kuliko binadamu asiye na shukrani.

Mtu ambaye alitakiwa anishukuru sana kwa juhudi zangu kwamba licha ya kuwa napokea mshahara kidogo niliweza kujinyima kwa kila hali ili niweze kumuandaa kuwa mke bora wa familia yangu hata wakati mwingine nashindwa kuwahudumia ndugu na rafiki zangu hatimaye naambulia matusi na dharau…inauma sana!!!!

Hakika uchawi binadamu wengine hawazaliwi nao ila machungu na maumivu wanayosababishiwa na binadamu wenzao huwafanya kuingia katika uchawi na ushirikina ili kutafuta faraja katika nafsi zao.
Kumbe inaweza isiwe zoezi gumu kubeba silaha na kutafuta uhai wa mtu au kumdhuru mtu, hii ni kutokana na binadamu kuwazamisha wenzao katika dimbwi la matatizo na majuto na wao wakakosa uwezo na hekima za kupambanua  Ukuu na Utukufu wa Mwenyezi Mungu katika kuchagua njia sahihi.

Lakini katika yote ushindi wa maamuzi unaweza kupatikana katika kile unachoamini hasa kufanya maamuzi ambayo hutojuta baadae . Hivyo, nilipiga moyo konde nikaomba hekima ya Mungu itawale katika maamuzi yangu na inipitishe kando katika mbigiri za kisasi zilizotanda moyo wangu nisahau yote.

Nashukuru kwa mapenzi ya Mungu niliweza kusahau na kusamehe yote yaliyopita nikawa bize na shughuli zangu za kutafuta maisha. Yaani tangu siku ile sikuwahi kumpigia simu wala meseji wala kumuulizia kwa jambo lolote yaani yeye na maisha yake na mume wake mimi bize na mambo yangu
Lakini cha ajabu hivi karibuni takribani miezi miwili iliyopita alinipigia simu na hii ni baada ya zaidi ya mwaka mmoja kupita pasipo kuwasiliana naye. Niliitazama simu nikaona ni namba ngeni lakini nilipopokea tu nilimtambua mapema kwa sauti yake.

Ambapo baada ya salamu alijikita moja kwa moja kuulizia maisha yangu…kabla sijamjibu chochote nilimuuliza, “Mbona bize na simu? Vipi huogopi kupoteza ndoa yako? Au sasa umeshaizoea?”
“Aaaaa!!! kawaida tu,” alinijibu kwa unyonge kabla hajaanza kuleta habari nyingine.

Niliongea naye kwa dakika kadhaa kisha nikakata simu na kuendelea na ratiba zangu..lakini tangia hapo amekuwa na mazoea ya kutaka kuongea nami hadi inafikia wakati analalamika kwa baadhi ya ndugu na rafiki zangu. Ndipo nilipopata taarifa zake kwamba ni kwa muda mrefu sasa wametengana na huyo mume wake…jamaa alimkimbia.

Itaendelea Kesho..!!!

Utunzi wa Edward Lucas; 0655 545 064

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad