Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya, IEBC, imeidhinisha majina ya wagombea nane kuwania Urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti mwaka huu
Kati ya wagombea hao, ushindani mkubwa unatarajiwa kuwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta anayewania muhula wa pili na mgombea wa muungano wa vyama vya upinzani NASA Raila Odinga.
Hata hivyo, zoezi la mchujo liliwaacha wengine zaidi ya 10 nje ya kinya'nga'nyiro hicho akiwemo Peter Solomon Gichira aliyefikishwa Mahakamani kwa madai ya kutaka kujiua baada ya kuondolewa katika orodha hiyo kwa kutokidhi vigezo.
Ushindani unaotarajiwa kati ya Rais Kenyatta na Bw. Odinga, unarejesha nchi hiyo katika historia ya siasa kati ya baba zao, Jomo Kenyatta aliyekuwa Rais wa kwanza na Jaramogi Oginga Odinga aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais baada ya Uhuru mwaka 1963.
Wagombea wengine sita ambao wanawania Urais ni pamoja na Cyrus Jirongo (UDP), Ekuru Aukot kutoka chama cha Thirdway Alliance, Abduba Dida (ARC).
Wagombea binafsi ni pamoja na Joseph Nyagah, Michael Wainaina na Japheth Kavinga, ambao wamejinadi kama chaguo sahihi la kuleta mabadiliko.