Nape Nnauye Amvaa Tena Mkuu wa Mkoa Sakata la Kuvamia Clouds Media
0
May 24, 2017
IKIWA ni miezi miwili imepita tangu kutokea tukio la uvamizi wa kituo cha Clouds Media Group na kuundwa kwa kamati ya kuchunguza tukio hilo, hatimaye aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amemvaa tena Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusema kwamba hakuunda kamati ya kumchunguza yeye, bali aliunda kamati ya kuchunguza tukio la kuvamiwa kwa kituo cha utangazaji cha Clouds Media Group.
“Niliunda kamati kuchunguza tukio la kuvamiwa kituo cha utangazaji sio kumchunguza RC. Kama RC alikuwa mmoja wa wavamizi, hayuko juu ya sheria,” ameandika Nape kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Alipoulizwa kwanini Waziri wa Habari aunde kamati ya uchunguzi wa tukio la uvamizi badala ya kamati hiyo kuundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Nape alijibu kwa kuuliza swali kama kila kamati inaundwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Majibu haya ya Nape yamekuja ikiwa ni saa chache baada ya kuulizwa ni yapi maoni yake kuhusu kauli ya Makonda kwamba hakuwa akifahamu mipaka yake ya kazi ndio sababu alikwenda kuunda tume ya kumchunguza.
Kauli ya Nape kuhusu kuunda kamati imekuja ikiwa ni takribani saa 24 tangu Makonda aliposema kuwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliunda kamati ya kumchunguza.
Makonda alisema hayo jana, ambapo alidai kuwa kamati iliyoundwa na Waziri isingeweza kumhoji kwa sababu haikuwa na uwezo huo kutokana na wajumbe wa kamati hiyo kutofahamu mambo yanayohusiana na masuala ya uvamizi.
Tags