Bunge la Afrika Mashariki (Eala) lililoanza kikao chake cha siku 14 jijini hapa na cha mwisho kwa Bunge la Tatu linalofikia ukomo Juni 4 limelitaka Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki kuharakisha uchambuzi wa kikosi kazi kilichoundwa kuchunguza ufisadi katika Sekretariati ya EAC.
Baada ya dua jana (Jumanne), Abubakar Ogle alisimama kwa kutumia kanuni za Bunge ibara ya 30 (l) inayompa mbunge uwezo wa kuwasilisha hoja mahsusi yenye masilahi kwa umma na kwa haraka, na baada ya kupewa nafasi alitaka Bunge lijadili mustakabali wa EAC baada ya taarifa ya uchunguzi kubaini ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Amesema kikosi kazi kilichoundwa licha ya kujiridhisha na tuhuma zilizojitokeza kulingana na taarifa ya mtumishi wa EAC aliyemaliza muda aliyedai kuna ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za jumuiya, pia kilibaini mambo zaidi ya yaliyotarajiwa ambayo yanafanya uhai wa EAC kuwa shakani.
Spika wa Bunge la Eala, Daniel Kidega alimtaka mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki ambaye ni Naibu Waziri wa Afrika Mashariki wa Uganda, Julius Maganda kujibu hoja hiyo.
Maganda amesema uchunguzi umekamilika ila bado haujawasilishwa kwenye baraza.
"Mheshimiwa Spika naliomba Bunge liwe na subira, tutakapokuwa tumepata taarifa kamili ya uchunguzi tutaifanyia kazi kwa kutoa mapendekezo kwa wakuu wa nchi za EAC," amesema Maganda
Wabunge walichangia hoja hiyo ni Bernard Mulengani, Dora Byamkama, Sarah Bonaya, Agnes Mumbi na Nancy Abisai, ambaye alionyesha hofu juu ya mustakabali wa jumuiya katika mazingira yanayoendelea katika Sekretariati ya EAC.
Patricia Hajabakiga, amesema vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya ofisi haviwezi kukubalika na jukumu la Bunge ni kusimamia mihimili mingine ili kuhakikisha utawala bora unakuwapo.