Imeelezwa kuwa Tanzania haijawekeza vya kutosha katika kilimo ili kukifanya kiweze kuendesha viwanda nchini.
Mwanasiasa mkongwe na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika katika Serikali ya Awamu ya Nne, Stephen Wasira amesema hayo na kuongeza kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kilimo na viwanda kwa sababu kilimo kinazalisha malighafi za kulisha viwanda na viwanda navyo, vinazalisha bidhaa au pembejeo za kukuza kilimo.
Katika mwaka wa fedha 2017/18, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inaomba Bunge kuiidhinishia Sh267.86 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.
Kati ya fedha hizo, Sh156 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh103 bilioni ni matumizi ya kawaida.
Wasira amesema Tanzania haiwezi kuendelea kiviwanda kama kilimo kitaendelea kuwa nyuma kama kilivyokuwa miaka mingi iliyopita.
Amesema kitu kikubwa kinachokwamisha ukuaji wa kilimo nchini ni teknolojia duni.
“Kilimo chetu kinakabiliwa na teknolojia duni, kwa mfano unaona watu bado wanavua kwa kutumia ndoano. Ilitakiwa tuanze kuvua kwa kutumia boti za kisasa ili kuongeza mazao ya samaki, kwenye kilimo hivyo hivyo,” amesema Wasira.