BENDERA pekee ya Marekani ilionekana jana ikipepea kwenye lango la kuingilia kwenye kasri la Papa Francis lililoko jijini hapa, wakati Rais wa Taifa hilo kubwa, Donald Trump alipowasili ikiwa ni siku yake ya tatu kutembelea vyanzo vya dini kubwa duniani.
Trump alikutana na Papa Francis katika siku yake ya tano ya ziara yake ya kwanza ya urais, baada ya kutembelea vyanzo vya dini za Uislamu na Uyahudi.
Wakati mazungumzo yao yakibaki siri, Rais huyo alikuwa na ujumbe mfupi kwa ajili ya Francis wakati akiondoka: “Sitasahau ulichokisema.
“Ni heshima kubwa,” alisema wakati akishika mkono wa Papa nao kupiga picha ya pamoja kwenye ghorofa ya pili ya Sala del Tronetto, ambacho ni chumba kidogo cha Utawala.
“Ahsante sana. Hii ni heshima kubwa sana,” Trump alisikika baadaye akisema wakati Francis amekaa upande wa pili wa dawati wakitazamana tayari kuanza mazungumzo yao, kwenye chumba chake cha faragha cha kujisomea.
Francis ambaye ni mtu asiyependa kufichaficha mambo, lakini wakati wote huo alikaa kimya.
Baada ya kutoka kwenye mazungumzo yao, Francis alionekana muda wote akitabasamu kila alipokutana na wana familia hiyo namba moja ya Marekani.
“Unampa chakula gani?” Francis alimhoji Melania Trump kwa Kiitaliano, akimaanisha jinsi Rais alivyo na umbo kubwa. “Pizza nyingi?” “Pizza!?” Melania aliuliza kwa mshangao huku akicheka.
Papa alibusu Rosari aliyokuwa nayo Melania mkononi, kabla ya kumsalimia Ivanka Trump na mumewe, Jared Kushner, sambamba na Waziri wa Mambo ya Nje, Rex Tillerson na maofisa wengine wa Marekani.
Baada ya mkutano na Papa, Melania alizuru hospitali ya watoto inayomilikiwa na Vatican. Alimwambia Francis: “Nimefarijika sana kutembelea hospitali hii ya watoto wachanga”.
Ziara ya Ivanka ilijumuisha pia kukutana na waathirika wa biashara ya binadamu na kuandaa mijadala mbalimbali na wanachama wa Jumuiya ya Sant’Egidio, kikundi cha kijamii cha kutetea haki cha Kanisa Katoliki.
Familia ya Trump ilikuja na zawadi mbili kwa ajili ya Papa, ikiwa ni pamoja na kasha la toleo la kwanza la vitabu vya Mchungaji Martin Luther King, Jr. “Nadhani utavifurahia,” alisema Trump.
Rais pia alimpa sanamu ya shaba nyeusi yenye maandishi ya ‘Panda Juu’, ikiwa na umbo la yungiyungi lililochanua.
Francis naye alijibu kwa kumpa medali kubwa iliyosanifiwa na msanii wa Kiroma – taswira ya mti wa mzeituni, kama alama ya amani.
“Tunaweza kutumia amani,” Trump alijibu. “Nimeisaini maalumu kwa ajili yako,” Francis alimwambia. “Ooh,” Trump alijibu. “Hiyo nzuri sana.”
Rais pia aliahidi kusoma nakala tatu za Waraka wa Baba Mtakatifu alizopewa na Francis – mojawapo ni ‘Lautado si’ yake, ambayo ni tasnifu inayozungumzia hifadhi ya mazingira. Zingine mbili zinahusu familia na Injili.