PROF. Lipumba: Niko Tayari Kuondoka CUF kwa Sharti Hili Tu..!!!


MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema yuko tayari kuondoka katika chama hicho ili kukiepusha na migogoro ikiwa tu mkutano mkuu utaamua, kama katiba yake inavyosema.

Mwenyekiti wa chama, kwa mujibu wa katiba ya CUF, alisema Lipumba anaweza kuondolewa madarakani kama wajumbe wengi wa mkutano mkuu wataridhia.

Prof. Lipumba alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku moja baada ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kusema hayuko tayari kupatanishwa naye kwa kuwa anatumiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuivuruga CUF.

Prof. Lipumba alisema endapo itathibitika kuwa uhai wa CUF unategemea yeye kuondoka, yupo tayari kufanya hivyo ila kwa mujibu wa katiba ya chama.

“Katiba ya CUF ipo wazi kuwa mwenyekiti wa CUF akitaka kufukuzwa, lazima theluthi mbili ya wajumbe wa Bara na theluthi mbili ya (wanaotoka) Zanzibar wampigie kura ya kukubali aondolewe," alisema msomi huyo wa uchumi.

Kumekuwa na mgogoro wa pande mbili CUF baada ya Profesa kujiuzulu uenyekiti kwa hiari yake Agosti, 2015 lakini akarudi miezi 10 baadaye, akidai hakuna kikao halali kilichopitisha uamuzi wake wa awali wa kujiengua kwenye nafasi hiyo.

“Huwezi kunifukuza uanachama," alisema Prof. Lipumba ambaye amefukuzwa uanachama na Baraza Kuu la CUF lakini akatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

"Kwanza kadi ninayo nyumbani, lakini Katiba yetu ipo wazi.

"Ukitaka kumfukuza mwenyekiti lazima uitishe mkutano mkuu na wajumbe wapige kura, na theluthi mbili Bara na Zanzibar wakubali.”

Alisema baada ya kuandika barua ya kutengua kujiuzulu na kumkabidhi Maalim Seif, naye alimshauri asianze kazi kama alivyoeleza katika barua ili aweze kushauriana na wanasheria wa chama, kitendo ambacho alikikubali.

Alisema Maalim Seif aliitisha mkutano mkuu ambao yeye hakuitwa na wakati ukiendelea baadhi wajumbe walimpigia simu kuwa barua yake inasomwa na kumtaka aende, ambapo alifanya hivyo.

Alisema ndani ya mkutano alikuta mjadala ambao wajumbe baadhi walimtaka mwenyekiti wa mkutano, Julius Mtatiro, aridhie Prof. Lipumba aitwe; ahojiwe lakini kiongozi huyo wa muda alikataa.

Alisema mkutano huo ulivunjika baada ya kutangazwa kura za kumkataa yeye, alisema Lipumba, "kura ambazo hazikupigwa".

KUVAMIA MIKUTANO
Mwezi uliopita watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Prof. Lipumba walivamia na kufanya fujo katika mkutano wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye yupo upande wa Maalim Seif.

Lakini Prof. Lipumba alisema hawana utaratibu wa kwenda kuvamia mikutano hiyo bali wapo wanachama wanaokaa katika maeneo husika wakiona chama chao kitaadhirika huenda kuhoji.

“Tukio lile la Kigogo (mwezi uliopita) lilinisikitisha," alisema Prof. Lipumba. "Sihusiki wala sikutoa maagizo watu wakavamie na kuwapiga waandishi wa habari kwenye mkutano wa CUF.”

Akizungumzia kesi iliyofunguliwa na upande wa Maalim dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na yeye, Prof. Lipumba amependekeza maamuzi yatakayofanyika pande zote mbili ziyazingatie.

Aidha, alimtaka Maalim Seif aelewe kuwa maridhiano lazima yawepo.

Pia alisema endapo Maalim Seif angeacha usultani na kuheshimu Katiba ya chama kusingekuwa na tatizo la msingi.

“Usultani wake niliandika barua ya kujiuzulu na kuandika barua ya kurudi katika nafasi yangu ambayo yeye alikuwa nazo lakini Maalim Seif aliitisha mkutano mkuu wa chama wakati barua ya kujiuzulu nimeshaitengua,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad