Rais John Magufuli ambaye yuko mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya siku tatu, jana alisali kwenye makanisa mawili; akianza na Kanisa Katoliki la Kristo Mfalme na baadaye kwenye Usharika wa Moshi Mjini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Hata hivyo, licha ya kuwaomba viongozi wa makanisa na wananchi wamuombee katika awamu ya uongozi wake, pia aliwataka waelewe mambo kadhaa yanayomfanya awe mkali, ingawa hana tabia hiyo.
“Nafikiri mnaweza kuona sura yangu nilipo hapa. Ni tofauti sana na inavyotafsiriwa. Inawezekana inatafsiriwa ni mtu katili, wa ajabu mkali, siko hivyo. Mimi ni mpole na mnyenyekevu,” alisema Dk Magufuli akiwa katika kabisa la Kristo Mfalme.
Kisha, Dk Magufuli aliainisha mambo yanayomweka katika hali ya ukali kuwa ni pamoja na rushwa, watumishi hewa serikalini, wizi, dawa za kulevya na maovu yote yaliyomo serikalini.
“Haya ninayoyafanya mimi na Serikali ni kwa sababu ya maovu makubwa yaliyokuwa yamejengeka ndani ya jamii na watu kutoogopa maovu,” alisisitiza huku akipigiwa makofi na waumini.
Mkuu wa KKKT, Dk Fredrick Shoo akamsifu kwa moyo wa kuthubutu kuyaanika majibu anayoyatumbua.
“Tunakuomba pale ambapo unatolewa ushauri kwa nia njema na washauri wema, Mungu akupe sikio la kusikia,” alisema Dk Shoo kauli ambayo iliamsha hisia za waumini wengi kanisani hapo.
Askofu Isaac Amani wa Kanisa Katoliki la Kristo Mfalme
Aliwataka Watanzania kuwa walinzi wa Taifa lao badala ya kuiachia jukumu hilo Serikali.
Leo, Rais Magufuli; Makamu wake, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa watawaongoza wananchi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kitaifa itafanyika mjini Moshi.