Rais John Magufuli amelitaka shirika la utangazaji la TBC, kutoa taarifa sahihi kwa watanzania bila kujali vyama vyao, dini zao wala makabila yao.
Pia Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na MichezoHarrison Mwakyembe aliyekuwepo katika ziara hiyo kuuangalia mkataba kati ya TBC na Star Times na kuchukua hatua zinazostahili endapo itabainika kuwa mkataba huo hauna manufaa.
Magufuli ameyasema hayo jana alipotembelea ofisi za Shirika hilo na kuwataka wafanyakazi wa TBC kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na ubunifu wa hali ya juu ili matangazo ya chombo hicho cha Taifa yawavutie Watanzania wengi, na kiwe chombo kinachoongoza nchini.
Magufuli ambaye hivi karibuni ametoa Sh3bilioni kwa ajili ya kuisaidia TBC amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dk Ayub Rioba kutumia fedha hizo kutatua matatizo ya uhaba na uchakavu wa vifaa vya uzalishaji wa vipindi na urushaji wa matangazo, kununua vyombo vya usafiri na kufanya ukarabati wa majengo.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi amewahakikishia kuwa Serikali itaboresha stahili zao kwa mujibu wa utaratibu uliopo na papohapo amemuagiza Dkt. Rioba kulipa mara moja malimbikizo ya posho zote ambazo wafanyakazi hao wanadai kuanzia Oktoba 2016, zilizofikia Sh3.2bilioni.
“Msemaji wa Serikali mkubwa ni TBC1 na Redio ya Taifa, nyinyi hamuwezi mkawa kama vyombo vingine ambavyo vina malengo yao ya kufanya biashara, nyinyi kazi yenu ni kutoa taarifa sahihi kwa Watanzania bila kubagua vyama vyao, bila kubagua dini zao, bila kubagua makabila yao, huo ndio uwe msimamo mkuu.
“Mmetoa mchango mkubwa sana kwenye Taifa hili, hilo ni lazima niseme, hata vipindi vyenu ukiviangalia ni vizuri vinaeleza mpaka maisha ya vijijini, na mimi ni shabiki mkubwa sana wa TBC, lakini tatizo lenu mnashindwa kwenda na wakati wa sasa.” amesisitiza Rais