RAIS Magufuli Atembelea TBC Taifa..Ataka Mkataba wa Star Time na TBC Uchunguzwe Haraka..!!!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 16 Mei, 2017 amefanya ziara katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo amekagua miundombinu ya shirika hilo na kuzungumza na wafanyakazi.

Mhe. Rais Magufuli amejionea jinsi miundombinu ya shirika hilo inavyokabiliwa na changamoto mbalimbali za uchakavu na teknolojia duni na amesema Serikali itafanyia kazi changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya ya studio za kisasa za kurushia matangazo katika makao makuu ya nchi Mjini Dodoma.

Hata hivyo Mhe. Dkt. Magufuli ambaye hivi karibuni ametoa Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuisaidia TBC amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt. Ayub Rioba kutumia fedha hizo kutatua matatizo ya uhaba na uchakavu wa vifaa vya uzalishaji wa vipindi na urushaji wa matangazo, kununua vyombo vya usafiri na kufanya ukarabati wa majengo.

Kuhusu maslahi ya wafanyakazi amewahakikishia kuwa Serikali itaboresha stahili zao kwa mujibu wa utaratibu uliopo na papohapo amemuagiza Dkt. Rioba kulipa mara moja malimbikizo ya posho zote ambazo wafanyakazi hao wanadai kuanzia Mwezi Oktoba 2016, zilizofikia shilingi Bilioni 1 na milioni 285.

Mhe. Rais Magufuli ametaka wafanyakazi wa TBC kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na ubunifu wa hali ya juu ili matangazo ya chombo hicho cha Taifa yawavutie Watanzania wengi, na kiwe chombo kinachoongoza nchini.

“Msemaji wa Serikali mkubwa ni TBC1 na Redio ya Taifa, nyinyi hamuwezi mkawa kama vyombo vingine ambavyo vina malengo yao ya kufanya biashara, nyinyi kazi yenu ni kutoa taarifa sahihi kwa Watanzania bila kubagua vyama vyao, bila kubagua dini zao, bila kubagua makabila yao, huo ndio uwe msimamo mkuu.

“Mmetoa mchango mkubwa sana kwenye Taifa hili, hilo ni lazima niseme, hata vipindi vyenu ukiviangalia ni vizuri vinaeleza mpaka maisha ya vijijini, na mimi ni shabiki mkubwa sana wa TBC, lakini tatizo lenu mnashindwa kwenda na wakati wa sasa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe aliyekuwepo katika ziara hiyo kuuangalia Mkataba kati ya TBC na Star Times na kuchukua hatua zinazostahili endapo itabainika kuwa mkataba huo hauna manufaa.



Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

16 Mei, 2017

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad