RAIS wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonatham amemshutumu Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama kwa kushindwa katika uchaguzi mkuu dhidi ya Rais wa sasa wa nchi hiyo Muhammadu Buhari, akidai kwamba aliongoza njama za ulimwengu dhidi yake ili kumwondoa madarakani.
Jonathan alitoa shutuma hizo katika kitabu kipya kilichotolewa Ijumaa iliyopita kinachoitwa Against The Run of Play, ambacho kinaeleza namna alivyokuja kuwa rais wa kwanza wa Nigeria aliyeko madarakani kushindwa katika uchaguzi.
Kuzuia machafuko
Alisema Obama na maafisa wake “waliweka wazi kwangu kimatendo kwamba walikuwa wanataka mabadiliko ya serikali nchini Nigeria na walikuwa tayari kufanya lolote kufanikisha nia yao hiyo. Waliweza hata kutuma meli za kivita kwenda katika Guba ya Guinea siku chache kabla ya uchaguzi,” alinukuliwa akisema katika kitabu hicho chenye kurasa 204, na mwandishi wa habari Olusegun Adeniyi.
Jonathan alipata sifa duniani baada ya kukubali kushindwa kabla ya matokea ya mwisho ya uchaguzi huo kutangazwa, jambo ambalo lilizuia machafuko makubwa ambayo yamewahi kutia dosari chaguzi za nyuma katika taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.
Alimshutumu Obama kwamba alimshawishi aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Rais wa sasa wa Ufaransa Francois Hollande kufanya kazi dhidi yake. “Nilikuwa napatana vizuri na Cameron lakini ilifika wakati, niligundua kuwa Wamarekani walikuwa wanamshinikiza na alilazimika kuungana nao dhidi yangu,” alisema.
“Lakini niligundua ni kwa kiasi gani Rais Obama alikuwa tayari kufanya ili kuniondoa mimi hadi Ufaransa nayo ikakubali kutokana na shinikizo kutoka kwa Marekani.” Jonathan alisema kuwa alikuwa na uhusiano mzuri na Hollande, ambaye alikuwa ni mtu wa kwanza kuwasiliana nae iwapo kunatokea matatizo katika nchi ya jirani ya Cameroon kuhusu kundi la Boko Haram.
Baada ya kutekwa kwa zaidi ya wanafunzi 200 wa kike kaskazini mashariki mwa mji wa Chibok nchini Nigeria, Hollande aliandaa mkutano wa usalama jijini Paris akizihusisha Nigeria pamoja na mataifa ya jirani.
Mazungumzo hayo yalikuwa ni muhimu katika kuunda jeshi la ukanda huo, ambalo limefanya kazi kubwa katika kudhoofisha sehemu hiyo ya kundi la Islamic State.
“Lakini wiki kadhaa kabla ya uchaguzi, aliungana na Wamarekani katika kuunga mkono upinzani dhidi yangu,” aliongeza, kulingana na kitabu hicho ambacho kimeonekana na shirika la habari la AFP.
Shutuma za rushwa
Chama cha Buhari cha All Progressives Congress (APC) kilimshutumu Jonathan kuwa alikuwa hafanyi inavyopasa katika kupambana dhidi ya tatizo la rushwa nchini humo. “Hilo ni jambo ambalo pia nilikuwa nikilisikia kwa Wamarekani bila kuwepo kwa shutuma za moja kwa moja dhidi yangu,” aliongeza, akipinga kwamba hakuwa amefanya lolote katika kupambana na tatizo hilo.
Buhari alimshutumu Jonathan na chama chake cha Peoples Democratic Party (PDP) kwa kuondoka serikalini na kuacha hazina ya nchi hiyo ikiwa “haina kitu”na kusema kuwa fedha nyingi za umma ziliibiwa.
Maafisa wa ngazi za juu wa PDP na utawala wa Jonathan, wakiwemo watu wa familia yake, kwa sasa wanakabiliwa na mashtaka ya rushwa.
Buhari, ambaye aliwahi kuongoza serikali ya kijeshi katika miaka ya 1980, ameshuhudia oparesheni zenye mafanikio dhidi ya Boko Haram, kundi ambalo limeua kiasi cha watu 20,000 nchini Nigeria pekee.
Rekodi mbaya ya haki za binadamu
Jonathan, ambaye utawala wake ulishutumiwa kwa kushindwa kuunga mkono na kutoa silaha nzuri kwa jeshi la nchi hiyo katika mapambano dhidi ya kundi la Boko Haram, anadai kwamba utawala wa Obama ulikuwa unadhoofisha jitihada za nchi yake dhidi ya Boko Haram.
Balozi wa Nigeria huko Washington mwaka 2014 aliishutumu Marekani hadharani kwa kukataa kuiuzia nchi yake helikopta za kivita. Jonathan alisema kwamba sheria za Marekani zinapiga marufuku mauzo ya silaha kwenda kwa mataifa ambayo yana rekodi mbaya ya haki za binadamu “kusababisha vita dhidi ya Boko Haram kuwa ngumu sana.”
Afisa wa ubalozi wa Marekani huko Abuja alisema kwa njia ya taarifa kwa vyombo vya habari kwamba “inashangaza” kwamba Jonathan anaonekana kuwa anabadili mtazamo wake katika uchaguzi. Sera za Washington kabla ya kura ilikuwa ni uchaguzi ambao ni huru, haki na wenye uwazi, alisema, na kuongeza kwamba Marekani iliamini kwamba matokeo yalikuwa ni “maoni na matakwa ya watu wa Nigeria.”