Kukoroma ni tatizo linalowapata watu wengi wakati wanapolala ambalo linaweza kuwatokea watu wa kila umri ingawa hutokea mara nyingi kwa wanaume au watu wanene. Kukoroma kwa kawaida sio tatizo kubwa na mara nyingi huleta tu karaha kwa mtu anayelala karibu na mkoromaji.
Mtu huwa anakoroma pale kunapokuwa na kitu au sababu yoyote itakayoziba kuingia au kutoka kwa hewa mdomoni na katika pua. Kuta za koo hutikisika wakati wa kupumua na matokeo yake ni sauti inayosikika ya kukoroma. Kuingia au kutoka kwa hewa huweza kuzuiwa na sababu mbalimbali kama vile.
Kuziba tundu za pua kusiko kamili ambako husababisha nguvu zaidi zitumike katika kupitisha hewa kwenye pua wakati mtu akiwa amelala. Kitendo hicho hupelekea nyama laini za pua na koo zijikusanye na kusababisha mkoromo. Kuna baadhi ya watu wanakoroma tu kipindi cha allergy (allergy season) au wanapatwa na matatizo ya sinus. Baadhi ya matatizo kama vile kupinda pua (deviated septum) au ukuta unaotenganisha tundu za pua na polyps za pua pia huweza kufanya pua zizibe na kusababisha kukoroma. Watu wengi wanaofanya operesheni za pua pia hupatwa na tatizo la kukoroma.
Kuwa na misuli dhaifu katika koo na ulimi. Misuli au nyama za koo na ulimi zinapokuwa dhaifu sana hulegea na kuanguka upande wa nyuma wa sehemu inayopita hewa. Suala hilo hutokea pale mtu anapolala fofofo au kuwa na usingizi mzito na kusababisha kukoroma.
Sababu nyinginezo zinazoweza kumsababishia mtu akorome anapolala ni kuwa na umri mkubwa au uzee, imeshuhudiwa kuwa watu wa makamo na wazee hukoroma, kwani misuli na nyama za koo huanza kuzeeka na kulegea kadri umri unayoongezeka.
Vilevile wanaume wanakoroma zaidi kuliko wanawake hii ni kutokana na wanaume kuwa na njia nyembamba zaidi ya hewa kuliko wanawake.
Kuondoka na hali hiyo mkoromaji yampasa kuzingatia mambo kama; kupunguza uzito, safisha njia ya koo ya hewa, Kuwa na pua iliyoziba hufanya kupumua kuwe kugumu na kusababisha kukoroma.
Unaweza kufanya hivyo kwa kutumia dawa za kusaidia kupumua kwa urahisi (nasal decongestants) zinazopatikana kwa urahisi katika maduka ya dawa pia kuaacha kuvuta sigara, kutokunywa pombe kabla ya kulala, au kutumia vinywaji au vyakula vyenye kafeini. Zingatia kulala mapema ili kupata muda wa kutosha kupumzisha mwili.