SAKATA la Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana Laibuka Bungeni...Ni baada ya Godbless Kulianzisha Huku Akidai Amefichwa..!!!


Kauli aliyoitoa bungeni juzi usiku mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amefichwa ilisababisha mawaziri wawili wa sasa na mmoja wa zamani wamkomalie kuifuta.

Bunge lilikuwa likijadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Awali, Lema alisema ameona kwenye mitandao juu ya Kinana kufichwa na kupaza sauti akitaka kumtetea akiwa kama Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani.

Hata hivyo, kauli hiyo ilimsimamisha Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene akitumia kanuni ya 64 (2) ambayo alisema inatoa nafasi kukumbusha Bunge kwamba kuna kanuni inayovunjwa.

“Mbunge anayezungumza anasema jambo ambalo hana uhakika nalo, linatia mashaka, sidhani kama ana uhakika kwamba Kinana amefichwa. Alithibitishie Bunge hili na kama hawezi kuthibitisha, kupitia kanuni ya 72 (2) nakuomba Mwenyekiti umtake afute maneno hayo,” alisema Simbachawene.

Ufafanuzi huo ulimuinua kitini Tundu Lissu na kusema Simbachawene hajui atendalo, Mungu amsamehe.

“Kanuni ya 72 (2) inasema mbunge atakayekiuka utaratibu uliowekwa na kanuni hizi anaweza kutakiwa na Spika hapohapo afuate utaratibu au mbunge atasimama kwa kutumia utaratibu huo na kutaja kanuni iliyokiukwa,” alisema Lissu.

Baada ya maelezo hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama ambaye ni mnadhimu mkuu wa Serikali aliweka msisitizo kwenye kanuni ya 64 (1) (a) ambayo inakataza mbunge kutotoa taarifa ambazo hazina ukweli.

“Naomba nimthibitishie mheshimiwa Lema kwamba Kinana tumezungumza naye wakati wa maadhimisho ya Muungano, wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi. Kinana ametoka kwenye matibabu na sasa anapumzika nyumbani kwake.

Alipomaliza kuzungumza Jenister aliinuka Mbunge wa Newala (CCM), George Mkuchika ambaye aliwahi kuwa waziri wa wizara mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Nne na kuomba mwongozo wa mwenyekiti kuwa tangu Lema aanze kuchangia hakuwa anazungumzia jambo lililoko mezani, yaani bajeti ya wizara ya habari.

“Mheshimiwa Lema tangu ameanza hakuzungumza habari zozote kuhusu wizara. Mimi kwa umri huu hata ukinizomea siachi kuzungumza. Mheshimiwa Mwenyekiti naomba muongozo wako kuhusu kanuni ya 64 (b) inayosema mbunge hatazungumzia jambo nje ya mjadala.

Akitoa mwongozo wake Mwenyekiti wa Bunge, Azzan Zungu alisema kwa mujibu wa kanuni hizi 68 (10) Spika ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu masuala yote ya kanuni, kwa hiyo akamtaka Lema afute maneno hayo na Lema aliyafuta akisema anafanya hivyo kwa kuwa waziri amemhakikisha kwamba Kinana hajatekwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad