SAKATA la Matumizi Mabaya ya Fedha ya Rambirambi za Wafiwa wa Wanafunzi 32 wa Shule ya Lucky Vincent Latinga Bungeni..!!


SAKATA la matumizi ya fedha ya rambirambi iliyochangwa kwa lengo la kuwafariji wafiwa wa wanafunzi 32 na wafanyakazi watatu wa Shule ya Lucky Vincent ya jijini Arusha, limetinga bungeni baada ya watunga sheria kutaka maelezo kwa nini fedha hiyo imeelekezwa kwenye matumizi ya serikali.

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), ndiye aliyelifikisha suala hilo bungeni mjini hapa jana aliposimama na kuomba mwongozo wa Kiti cha Spika kuhusu matumizi ya fedha hizo mara tu baada ya kumalizika kwa kipindi cha 'Maswali na Majibu'.

Katika kujenga hoja yake, mbunge huyo alisema amepata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba, fedha ya rambirambi imeelekezwa katika ukarabati wa Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha.

"Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo wako kwa kutumia Kanuni ya 68(7) kinachohusu jambo lilijitokeza mapema bungeni. Nilikuwa hapo nje, nimeangalia magazeti yanaelezea matumizi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya rambirambi na kuwafariji wafiwa wa watu waliofariki katika ajali ya basi la Shule ya Lucky Vincent zimetumika kinyume cha malengo yake," alisema.

“Madaktari wamelipwa kama posho na fedha zingine zinakarabati Hospitali ya Mount Meru, tofauti na ilivyokusudiwa. Katika hili, Bunge linahusika kwa maana tulikatwa posho hapa ili kusaidia familia za wafiwa, ilikuwa misaada kwa wahusika. Sasa hii tabia imekuwa ikijirudia."

Alisema wananchi wamekuwa wakichanga kwa lengo la kusaidia waathirika lakini serikali imekuwa haifikishi fedha hizo kwa walengwa.

"Tabia hii imekuwa ikijirudia mara kwa mara, jambo ambalo si zuri kwani watu wataacha kuchanga wakijua kwamba fedha hazisaidii walengwa," alisema na kufafanua zaidi:

"Tabia hii inanikera hata mimi mwenyewe, kama tutakuwa tunachanga fedha za rambirambi halafu inabadilishwa matumizi juu kwa juu bila hata wahusika kupelekewa.

"Kama ni hivyo, ni vyema kila chama kikakusanya fedha za michango chenyewe au kada zingine zifanye hivyo kwa lengo la kuwafikishia wahusika wenyewe ili kuepuka ulaji wa fedha za michango."

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, akimjibu mbunge huyo, alisema chombo hicho cha kutunga sheria hakiwezi kufanyia kazi kupitia taarifa za vyombo vya habari.

Chenge pia alisema: “Kwa mila na desturi za kiafrika, ukishatoa mchango wako wa rambirambi unawaachia familia ile au chombo kile... sijatoa mwongozo haya ni maoni yangu."

"Naomba tusiendeleze jambo hilo, serikali ipo, Bunge lipo, unategemea mrejesho ili siku nyingine mkiombwa iwe rahisi kutoa lakini kuleta tuhuma tu, siyo.

“Ila kwa mwongozo wangu, swala lako halijatokea mapema bungeni leo (jana). Kwa hiyo, sina cha kulijibia, hatuendeshwi na magazeti humu bungeni."

Bunge lilichangia Sh. milioni 100 (wabunge Sh. milioni 86 na Ofisi ya Bunge Sh. milioni 14) kwa lengo la kuwafariji wafiwa.

Michango iliyotolewa na wadau ni zaidi ya Sh. milioni 300, Sh. milioni 133 zikitolewa kwa familia za wafiwa (kila familia ilipata Sh. milioni 3.8).

Wanafunzi 32, walimu wawili na dereva walifariki katika ajali ya barabarani baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kutoka mjini Arusha kwenda Karatu kufanya mitihani ya ujirani mwema, kudaiwa kupinduka na kuingia kwenye korongo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad