Katika mahubiri yake Jumapili ya jana, Askofu Gwajima alimpongeza Rais Magufuli kwa hatua alizochukua na kumtaka azidi ‘kukaza uzi’ kwani Watanzania tunashangaza kuishi kwenye umaskini licha ya nchi yetu kujaliwa rasilimali nyingi ambazo kama zingetumika kwa usahihi tungekuwa tunaogelea kwenye utajiri.
Askofu Gwajima alisema haiwezekani nchi yenye madini mengi zaidi ya 320 anayoyajua, wingi wa mito, maziwa na mbuga za wanyama, lakini bado inaomba msaada ikiwemo wa chakula kutoka kwa mataifa ambayo kwa uhalisia yalitakiwa kuomba msaada kutoka kwetu.
“Nataka niseme ukweli pasipo kupindisha mambo kuwa, sisi Watanzania tumerogwa na mchawi wetu ni special (maalum), kwa sababu haiwezekani kwa nchi yenye utajiri mkubwa kama huu, madini, maziwa, mito, mabonde na mambo mengine yenye kuvutia ikiwemo mbuga za wanyama, lakini bado wananchi wake wanauza karanga na ubuyu, huko ni kurogwa.
“Nampongeza sana Rais Magufuli kwa kuamua kukata utepe ambao ulikuwa umedumu kwa muda mrefu, eti wachimbaji wachukue asilimia zote za madini na kutuachia asilimia nne tu, inaingia akilini kweli? Kuna aina 320 za madini ninayoyajua, mengine hata ukitajiwa majina unabaki unashangaa, sasa watu wanakuja na kuchukua yote, huku sisi tunabaki maskini, sasa kama siyo kurogwa huko ni nini? Watanzania tumerogwa, wewe zaidi ya makontena 277 yalitakiwa yapelekwe nje, hakika tumerogwa na tunatakiwa tuamke sasa,” alisema Askofu Gwajima.