Nimesoma ripoti maalum ya Gazeti wiki la Jamhuri la Leo Jumanne, Mei 9, 2017 yenye kichwa cha habari 'Zitto Anyukwa' inayohusu uchunguzi wa gazeti hilo juu ya ununuzi wa ndege ya Dreamliner kutoka shirika la ndege la Beoing, ununuzi ambao binafsi kwa nafasi yangu ya ubunge unaonipa mamlaka ya kuisimamia serikali, nimeutulia mashaka na kuomba maelezo zaidi ya serikali bungeni juu ya ununuzi huo.
Nawapongeza sana Waandishi na Wahariri wa Gazeti hili Kwa kufanya uchunguzi kuhusu suala la manunuzi ya ndege Hii ya Boeing 787-8 Dreamliner. Magazeti ya habari za uchunguzi ni taasisi imara na muhimu mno katika kujenga utamaduni wa uwazi, uwajibikaji na uadilifu nchini, utamaduni ambao Chama chetu cha ACT Wazalendo kinapigania kuusimika nchini. Gazeti la Jamhuri limethubutu kufanya vile wengine wameshindwa kufanya.
Gazeti la Jamhuri limeibua masuala mawili muhimu sana katika ripoti yao hii maalum, mosi limeeleza kuwa ndege inayonunuliwa ni mpya kabisa, ambayo bei yake kwa mujibu wa taarifa rasmi za Shirika la ndege la Beoing ni Dola za Kimarekani milioni 224.6 (zaidi ya shilingi bilioni 450), pili jamhuri wameeleza kuwa pamoja na kununua ndege mpya kabisa (ambayo bei yake ni zaidi ya shilingi bilioni 450) bado tumeuziwa ndege hiyo 'mpya kabisa' kwa bei ya dola milioni 150 (zaidi ya shilingi bilioni 330).
Baada ya kusoma ripoti husika, nimepata maswali muhimu yafuatayo yanayopaswa kujibiwa na Serikali (na naamini Jamhuri watatusaidia kuyauliza):
1. Jamhuri wanasema bei ya 'ndege mpya' ambayo si 'terrible teen' (zile zenye matatizo ambazo wenzetu duniani wameuziwa kwa bei ya chini), kwa mujibu wa mkataba waliouona Kampuni ya Boeing na Serikali ni dola za Kimarekani milioni 150 (zaidi ya shilingi bilioni 330) na si dola milioni 224.6 (zaidi ya bilioni 450) inayosemwa na Serikali. Bei sahihi ya 'ndege mpya' ni ipi kati ya hizo mbili?
2. Kwa mujibu ya Randama ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mawasilisho ya Bajeti ya mwaka 2017/18, ambayo iliwasilishwa kama Taarifa ya Waziri wa Wizara husika, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa kwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Serikali ilieleza kuwa imeilipa Kampuni ya Beoing kiasi cha dola milioni 67 (zaidi ya shilingi bilioni 134) ambazo ni 30% ya bei ya dola milioni 224.6 ambayo ndiyo bei ya ndege mpya kwa mujibu wa Boeing wenyewe (na kwa mujibu wa Serikali yenyewe Bungeni). Je Serikali mpaka sasa imelipa 30% ya $224.6m ambayo ni $67 (kama ilivyosema yenyewe) au imelipa 30% ya $150m ambayo haiwezi kuwa hiyo $67m.
Binafsi nimeomba Mkataba husika kwa mujibu wa sheria na taratibu za kibunge. Tukipata tutawajulisha. Lengo letu la kuhoji ni kupata ukweli, kujiridhisha na kusimamia matumizi sahihi ya fedha na rasilimali za umma kwa mamlaka tuliyopewa nanyi wananchi.
Hatuna nia mbaya Kabisa na mchakato wa kuboresha Shirika letu la Ndege la Taifa. Uboreshaji huu ulikuwa ni msimamo wa Chama chetu kwenye ilani yetu ya uchaguzi. Tunao wajibu wa kuhakikisha unafanyika kwa usahihi.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini - ACT Wazalendo
Mei 9, 2017
Dodoma